Mgogoro wa CUF umeingia katika sura mpya baada ya viongozi waliosimamishwa uanachama kutishia kumshtaki Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro wakitaka athibitishe kama walihusika katika jaribio la kumteka nyara Kaimu Naibu Katibu Mkuu (Bara), Joram Bashange.
Viongozi hao ni aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Magdalena Sakaya na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya.
Agosti 29, viongozi hao walisimamishwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwenda kinyume na Katiba ya chama hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Kambaya alisema tuhuma hizo ni nzito kwao na suluhisho pekee ni kumfikisha Mtatiro mahakamani ili akathibitishe alichokizungumza.