Kiungo wa zamani wa Manchester United Paul Scholes amemshauri Paul Pogba kufanya mambo yawe rahisi badala ya kumuiga staa wa Barcelona Lionel Messi.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mpaka sasa amekuwa na wakati mgumu tangu arejee Old Trafford kufuatia uhamisho wake uliovunja rekodi ya dunia kutoka Juventus, huku akikosolewa vikali na baadhi ya mashabiki siku za hivi karibuni.
Scholes anaamini kwamba Pogba anakazana sana kuonesha utofauti, lakini amemshauri kiungo huyo kuelekeza akili zake zote kwenye mchezo na kufanya kama alivyokuwa akifanya Italy.
“Pogba anaonekana kucheza sehemu ndogo sana ya uwanja. Nadhani anatumia muda mwingi sana kukaa na mpira,” Scholes aliiambia BT Sport kufuatia United kupoteza mchezo wao dhidi ya Feyenoord kwa 1-0 kwenye Ligi ya Europa.
“Anataka kupiga chenga wachezaji watatu mpaka wanne. Anatembea sana na mpira. Anachotakiwa kufanya ni kujitahidi kutokakaa na mpira. Huyo sio mchezaji ambaye Manchester United walimhitaji. Hawakumnunua mchezaji mithili ya Messi ili aje kupiga chenga wachezaji watano. Wamenunua kiungo mwenye nguvu na imara ambaye anaweza kunyang’anya mipira.
“Ana ujuzi, anaweza kutembea na mpira na anaweza kupiga pasi vizuri. Kama anakokota mpira mara moja au mbili halafu anapiga pasi kwa Zlatan [Ibrahimovic] halafu anaomba tena pasi, hakuna mtu ambaye ataweza kumkaba. Ana kasi nzzuri sana pamoja na nguvu kubwa.”
Scholes anaamini kwamba kucheza mbele ya kiungo mtulivu Michael Carrick kunaweza kuwa na faida kubwa sana kwa Pogba.
Aliongeza: “Nadhani Pogba anahitaji aina hiyo ya uchezaji kama alivyokuwa akifanya Juventus. Ni kiungo mweye uwezo mkubwa wa kuudhibiti mchezo na endapo akipewa Michael Carrick nyuma yake basi mambo yatakuwa safi.”