SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 21 Septemba 2016

T media news

Mwenyekiti UVCCM Arusha bado ang’ang’aniwa

KAMATI ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), imependekeza kwa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumvua uongozi Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya kutokana na kesi iliyofunguliwa mahakamani.

Uamuzi huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Sadifa Juma Khamis walichokutana juzi.

Shaka alisema wakati ikisubiri maamuzi ya Kamati Kuu, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa, imemsimamisha uongozi wa nafasi yake ndani ya UVCCM.

“Kuanzia leo tarehe 20/09/2016 asijihusishe na shughuli zozote za uongozi wa UVCCM hadi hatima ya tuhuma zake itakapoamuliwa na Mahakama na vikao husika vya UVCCM na CCM,” alisema Shaka.

Aliongeza kuwa kwa nyakati tofauti, Sabaya alisimamia na kuyaongoza makundi ya Vijana wa CCM na wasiokuwa wa CCM ili kumkataa Katibu wa UVCCM aliyehamishiwa mkoani Arusha, Said Goha. Alisema Sabaya alisababisha taharuki iliyofanya ofisi ya UVCCM Mkoa wa Arusha, kufungwa kwa minyororo hadi Jeshi la Polisi kuingilia kati.

“Taharuki hiyo ilichangia kwa kiasi kikubwa vijana wa Mkoa wa Arusha kugawanyika katika makundi na kupelekea hali ya Kiusalama na Maadili kwa Jumuiya na Chama kuwa ya wasiwasi,” alisema.

Alisema Sabaya amefikishwa mahakamani, akikabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kujifanya mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa huku kosa la pili akidaiwa kughushi vitambulisho vya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) chenye namba MT 86117 wakati akijua ni kinyume cha Sheria za nchi.

“Kwa makosa yote hayo, Lengai ole Sabaya ameyafanya kwa kukiuka Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM Fungu la 3 Ukurasa wa 16 na 17, na Fungu la 4 Ukurasa wa 29, 30 na 31. Pia makosa hayo ameyatenda kinyume na taratibu za Uongozi na Maadili za UVCCM Ibara ya 6.3.2 Ibara ya 7.5.1, 7.5.4 na 8.2.5,” alisema.

Pia Shaka alisema Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa, imebariki maamuzi yaliyochukuliwa na Sekretarieti ya Baraza Kuu la Umoja huo, iliyopendekeza kwa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kumfukuza kazi mara moja aliyekuwa Katibu wa Umoja huo Mkoa wa Arusha, Ezekiel Mollel.

Shaka alisema uamuzi umefikiwa kutokana na Mollel kukosa adabu pamoja na kukiuka kanuni za maadili ya chama hicho pamoja na kukataa uhamisho, aliopatiwa na uongozi wa juu wa umoja huo, hivyo kukiuka Kanuni ya Utumishi ya UVCCM Kifungu cha 3(13) Ukurasa wa 21 na 22, inayozungumzia uhamisho wa mtumishi.