Mlinda mlango wa Mbeya City Juma Kaseja amesema yeye si mkongwe kama watu wengi wanavyomwita na kumwambia astaafu soka, badala yake amewajibu kwamba, yeye bado anadai kwasababu alianza kucheza soka mapema na hana mpango wa kustaafu kutokana na maneno ya watu.
Golikipa huyo aliyetamba na klabu ya Simba na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ amethibitisha kuwa yeye bado ni mchezaji halali wa Mbeya City licha ya kutoonekana na kikosi hicho cha jijini Mbeya tangu kuanza kwa msimu huu.
“Mimi si mkongwe kama watu wanavyozungumza, nilianza kucheza mapema na nikapata nafasi kubwa ya kucheza. Kuna watu wengi niliwakuta kwenye soka na leo hii bado wanacheza lakini nashangaa watanzania wanasema Juma ni mzee anatakiwa astaafu. Juma Kaseja ni mdogo alianza kucheza mapema, siwezi kutoka kwenye soka kwasababu watu wanaongea”
“Tulishacheza timu kubwa tuwapishe wengine wacheze lakini mpira bado naendelea kucheza na ntacheza sana kuliko hao wadogo wanaoambiwa wacheze katika hizo timu kubwa.”
“Imekuwa kama kasumba kwenye mpira wa Tanzania ukicheza miaka mitatu, minne watu wakishakuchoka wanazungumza wanavyotaka wao. Na style ya kuwaondoa watu kwenye soka ni kuwaambia wamezeeka, inawaondoa wengi wachezaji wengi.”
Kaseja amekosa mechi zote za Mbeya City lakini anasema alikuwa anaruhusa maalumu kwa ajili ya kuisaidia timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys.
“Mimi ni mchezaji wa Mbeya City kwasababu kwenye usajili jina langu lipo na nadhani ntajiunga na timu hivi karibuni.”
“Nilikuwa naruhusa maalum niliondoka na timu ya taifa ya vijana kwenda kuwasaidia nikarudi nikakuta timu ipo Mwanza ilienda kucheza mechi, nisingeweza kujiunga na timu ikiwa Mwanza kwasababu ilikuwa imeenda kucheza mechi. Nikirejea kutoka timu ya taifa ya beach soccer, najiunga na timu yangu.”