SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 19 Septemba 2016

T media news

KILIO Cha Maalim Seif Chafikishwa UN


Maalim Seif

ZIARA ya kimataifa aliyoifanya Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Marekani, Ulaya, Canada na Umoja wa Mataifa kulalamikia uvurugaji wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba mwaka jana, imeanza kuzaa matunda, anaandika Jabir Idrissa.

Tayari taasisi ya kimataifa ya umoja wa wanaliberali – Liberal International (LI) – imeliandikia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) kutaka kutolewa kwa vikwazo dhidi ya Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kwenye tovuti ya LI, taasisi hiyo imetaka baraza hilo lenye jukumu la kulinda misingi ya haki za binadamu kwenye mataifa yote wanachama wa UN, kuchukua hatua kali ili kukomesha “uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukandamizaji wa haki za kisiasa na kiraia visiwani Zanzibar.”

Katika tamko walilolitoa na kufikishwa mbele ya Mkutano wa 33 wa Baraza hilo uliofanyika Septemba mosi mwaka huu, Liberal International imetaka jumuiya ya kimataifa, kufikiria kuweka vikwazo vya kusafiri na kuzuia mali za watu wote walioshiriki kuidhinisha vitendo vya utesaji wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao.

Taasisi hiyo ambayo CUF ni mwanachama wa muda mrefu, imetoa wito kwa wabunge wanaofuata mtizamo wa kiliberali walioko upande wa serikali na upinzani katika mataifa yote duniani kuchukua msimamo imara kupitia mabunge ya nchi zao na kutoa matamko ya kupinga walichokiita “uonevu wanaofanyiwa viongozi wa upinzani Zanzibar na wafuasi wao.”

“Tunaitaka serikali ya Zanzibar na Tanzania kuheshimu utawala wa sheria na kuingia katika majadiliano na upinzani ndani ya muda maalum hatua ambayo itawezesha kuundwa serikali ya mpito na kukubali kuitishwa kwa uchaguzi mpya ili kuondoa mgogoro uliojitokeza baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015,” imesema taarifa ya LI.

Hatua hiyo ya LI kuandikia Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa inakuja wiki kadhaa baada ya Maalim Seif kukutana na taasisi mbalimbali za kimataifa zinazoshughulikia maendeleo ya demokrasia na utawala bora, pamoja na wakuu wa serikali za Marekani, Ulaya na Canada.

Maalim Seif aliyefuatana na baadhi ya wasaidizi wake pia alifika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague, Uholanzi ambako aliwasilisha malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa Zanzibar kwa idhini ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua ya Maalim Seif na CUF imekuja baada ya CCM kumuamuru Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, 28 Oktoba, baada ya kubaini kuwa chama hicho kimepoteza madaraka kupitia sanduku la kura.