Ukifungua vitabu vya kumbukumbu kuhusu soka, utalikuta jina la Nereo Rocco. Rocco ndiye mwanzilishi wa soka la kujilinda zaidi kuliko kushambulia maarufu kama Catenaccio. Alipokuwa AC Milan mwaka 1963 alishinda ubingwa wa Ulaya kwa staili hii ya kucheza kwa kujihami.
Kama alivyowahi kusema baba wa lugha ya Kingerezea William Shakespears kwenye shairi la Venuis and Adoins, Seed spring from Seed. Basi Rocco ni mbegu ambayo imezalisha mbegu nyingine nyingi ambazo hufuata falsafa zake kwenye dunia ya leo.
Huwezi kubezwa kule nchini Italia kama timu yako inacheza kwa kujilinda. Kumbuka staili hii ilimpa ubingwa wa Uefa Jose Mourinho alipokuwa na Inter Milan. Mbegu ya Rocco imezalisha wachezaji wagumu mfano wa kina Genaro Gattuso. Pia imeleta makocha wanaopenda kutumia wachezaji wagumu ambao ni imara sana pindi timu inapotaka kujilinda.
Mmoja wa zao ambalo limetokana na mbegu aliyopanda Rocco zaidi ya miaka 50 iliyopita ni kocha wa Chelsea, Mtaliano Antonio Conte. Conte ni muumini wa soka la kibabe, yeye mwenyewe alikuwa yupo hivyo wakati anacheza kwenye klabu ya Juventus.
Kuthibitisha kuwa anapenda soka la kitemi angalia wachezaji ambao walihusishwa kujiunga na Chelsea wakati wa dirisha lililopita. Akiwa tayari amemsalia Ng’olo Kante kutoka Leicester City, bado alitaka kumleta Raja Naigollan lakini Roma wakagoma. Kama angeafinikiwa kumsajili Raja Naigollan basi Chelsea ingekuwa na viungo wanne wa ulinzi.
Takribani mechi tano za ligi kuu nchini Uingereza zimechezwa hadi sasa, Conte anaendelea kuwatumia Kante na Matic kwa wakati mmoja. Iwe kwenye mechi dhidi ya timu dhaifu au Ngumu bado shepu ya kikosi cha Chelsea ni ile ile chini ya Conte.
Falsafa hizi za Rocco zinamfanya kiungo wa kihispaniola Cesc Fabregas kuwa moto unaoanza kugeuka jivu taratibu chini ya kocha Antonio Conte. Licha ya ubora alionao bado hana nafasi hata kwenye mechi ya Cheslea dhidi ya Watord. Hadi sasa Fabregas amecheza dakika thelathini na sita tu akiwa na assist moja ya bao.
Fabrgeas anaponzwa na staili yake ya uchezaji, kwa bahati mbaya alikulia kwenye chuo kinachofundisha mpira laini, La Masia kule Catalunya jijini Barcelona. Conte anamuona Fabregas sio askari sahihi atayemsaidia kushinda vita ya kurudisha heshima ya Chelsea ambayo ilipotezwa na Jose Mourihno kwenye msimu uliopita. Amekuwa hajali sana assist za Fabregas wala mabao mabao yake maridadi.
Fabreags amekuwa mchezaji wa Mpango B baada ya timu kushindwa kupata matokeo. Mfano ni mechi dhidi ya Swansea pamoja na Liverpool, baada ya timu kuwa nyuma na mpango A kufeli ndipo Conte anampa nafasi Cesc Fabregas kwenda kubadilisha matokeo.
Chelsea bado haijafanya vibaya tangu kuja kwa Conte lakini kuna buruadani ambayo imeanza kupotea kwenye mboni za macho yetu. Mabadiliko ya benchi la ufundi pale Stamford Bridge yametunyima kuona pasi za mwisho za Cesc Fabregas. Kumbuka huyu ndiye mchezaji anayeshikilia rekodi ya muda wote kupiga pasi za mabao kwenye EPL.