Na Baraka Mbolembole
UNAPOZUNGUMZIA soka la Tanzania hivi sasa bila shaka utalitaja jina na mshambulizi, Mbwana Samatta ‘Samagooal77.’ Kijana huyo mwenye miaka kwa sasa anacheza soka la kulipwa katika klabu ya KRC Genk ya Belgium Pro League.
Hadi kufika, Ubelgiji, Samatta alianza kuonyesha uwezo wake katika timu ya Mbagala Market mwaka 2009 na alishinda tuzo binafsi ya ufungaji bora katika ligi daraja la kwanza. Magoli yake 16 yaliisaidia timu hiyo kupanda hadi ligi kuu Bara na msimu wake wa kwanza katika VPL akafanikiwa kufunga magoli 6.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa 2009/10, Samatta akasajiliwa Simba SC lakini kwa sababu za kimaslai kijana huyo akalazimika kusubiri hadi mwanzoni mwa mwaka 2011 kuanza kuichezea Simba. Ndani ya miezi mitatu akafanikiwa kufunga magoli 8 katika VPL na mengine manne katika Caf Champions League.
Mei, 2011 Simba ilimuuza mchezaji huyo kwa usajili wa rekodi kwenda TP Mazembe ya DR Congo na huko akatumia miaka minne kufanya mambo makubwa.
Hadi anasajiliwa Genk Januari mwaka huu, Samatta alikuwa na tuzo ya mwanasoka bora wa ndani ya Afrika 2015, mfungaji bora wa Champions league huku pia akiwa mshindi wa mataji mawili ya ligi ya DR Congo na lile la ligi ya mabingwa.
Baada ya Mazembe kumaliza ushiriki wake katika klabu bingwa ya dunia, Desemba 2015, Samatta alishinikiza kuuzwa na klabu pekee aliyoitaka ni Genk licha ya Moise Katumbi (mmiliki wa Mazembe) kuzungumza na kufikia mwafaka na timu ya Standard Liege pia ya Ubelgiji.
Baada ya kutua Genk, mshambulizi huyo wa Taifa Stars alifunga magoli matano msimu uliopita na kuisaidia timu yake kufuzu kwa michuano ya ligi ya Ulaya ‘Europa League.’
Msimu huu Mtanzania huyo ameanza vyema, akiwa tayari amefunga magoli 8 (manne katika ligi kuu na mengine manne katika hatua ya mtoano ya Europa)
Watanzania wengi wamekuwa wakifuatilia maendeleo yake na jana Jumapili, Samatta hakuwapo hata katika orodha ya wachezaji wa akiba wa timu yake ilipopoteza 2-0 mbele ya vigogo Anderletch.
“Ninasumbuliwa na goti la mguu wa kulia.”anasema Samatta nilipofanya naye mahojiano akiwa Ubelgiji leo Jumatatu.
“Nilipata maumivu hayo katika game ya Europa (Rapid Vienna 3-2 Genk) Leo nimefanyiwa vipimo na inaonesha tatizo sio baya. Nitakuwa nje ya uwanja kwa siku nne mpaka 7 itategemea ni kiasi gani mwili utakavyokuwa.”
Nilimuuliza pia Samatta sababu ya yeye kuanza vizuri msimu huu na hakusita kusema,
“Maandalizi mazuri kabla ya kuanza msimu yamenisaidia kwa kiasi kikubwa. Kuwa pamoja na timu kipindi cha maandalizi ya msimu mpya kimenisaidia sana kuwajua wachezaji wenzangu, na wao wamenijua vizuri.”
“Ni kipindi ambacho mnakuwa pamoja muda mwingi kwa maana mnaweza kufanya mazoezi mara mbili au mara tatu kwa siku. Mnabaki pamoja kabla ya mazoezi mengine hivyo mnajenga kujuana vyema na kutambua aina ya kila mchezaji kiundani.”
Katika safu ya mashambulizi ya Genk kila mshambuliaji ni mmaliziaji mzuri lakini Samatta ameweza kuingia katika timu ya wachezaji 11 haraka sana ukizingatia na nchi anayotoka.
“Pamoja na uwezo wangu wa kufunga lakini pia uwezo wa kuusoma mchezo na kuwaongoza wengine ni kitu kinachonisaidia sana kuingia katika kikosi cha kwanza. Malengo yangu msimu huu ni kufunga magoli yasiyopungua 20 katika michuano yote.”
Kucheza michuano ya Ulaya, kumekuongezea chochote? “Michuano ya Ulaya ni mikubwa sana imeniongezea experience na kujiamini pia.”