MTUNZI: ENEA FAIDY
....BI CAROLINA alipiga hatua za taratibu kuelekea sebuleni lakini hali iliyokuwemo ndani mle ilizidi kumshangaza kwani alisikia harufu Kali na mbaya ya kitu kuungulia. Alifika sebuleni lakini hakukuta Mtu yeyote, akaamua kwenda jikoni.
Alipoingia jikoni tu, alipiga chafya tatu mfululizo kutokana na moshi mzito ulioambatana na harufu Kali sana uliotawala jikoni mle. Aliisogelea mpaka sehemu ya kupikia akagundua moto uliwashwa na kuna kitu kilichomwa. Akaangalia sufuria zote lakini hakukuta kitu chochote, akabaki na mshangao.
"Doreen!" Aliita Bi Carolina akiwa ameshika mkono kiunoni.
"Abee mama!" Sauti ya Doreen ilisikika kutoka chumbani.
"Njoo huku jikoni"
Bila ya kuchelewa Doreen alifika jikoni kule na kumkuta Bi Carolina akiwa ameshika kiuno akimsubiri kwa hamu amuulize kilichotokea.
"Abee mama" aliitikia Doreen kwa adabu sana.
"Nini kimetokea huku jikoni?"
"Nisamehe mama... Nilitaka kupika.. Ila kwa bahati mbaya nikaunguza kwani sijui kutumia jiko la gesi." Alijitetea Doreen huku akitia huruma sana.
"Ulitaka upike nini asubuhi yote hii?"
"Nili...nilikuta maziwa.. Nyama kwenye friji nikataka nipike.."
"Mara maziwa mara nyama.. Mbona sikuelewi? Haya ulipikia sufuria gani?" Bi Carolina alishindwa kumuelewa Doreen ila kutokana na ugeni aliokuwa nao hakuweza kumfokea sana kwa kuhofu kuwa atajisikia vibaya.
"Nilichukua nyama... Sufuria ilipoungua sana nikaamua kuiosha.." Alisema Doreen akidai kutetemeka kwa woga.
"Sawa ila usirudie tena.. Nitakufundisha jinsi ya kupikia jiko la gesi.."
"Sawa mama" alisema Doreen kwa sauti ya upole iliyojaa hekima ya viwango vya juu.
"Sawa mwanangu nenda kaendelee na kazi zako"
Doreen alitoka jikoni mle na kuelekea chumbani kwake. Alichukua kimfuko cheusi kidogodogo kisha akafungua na kuutoa ungaunga mweusi. Kisha akaweka kiganjani na kusogelea kila kona ya chumba kile na kuupuliza kwa midomo yake. Alifanya hivyo mpaka unga ule ilipoisha, akasogelea kitanda chake na kukaa.
"Hapa sasa nimemaliza kazi... Mpaka huo moshi uishe nitakuwa nimefanikiwa kabisa." Alisema Doreen akitabasamu kwani ule moshi uliotapakaa ndani mle ulisababishwa na Doreen. Alikuwa amechoma dawa ambayo ingewafanya wakaaji wa nyumba ile kumpenda Doreen kupita kiasi, na wasingeweza kumfukuza hata iweje mpaka pale atakapoamua kuondoka yeye mwenyewe.
Aliangalia SAA yake ya mkononi ilikuwa tayari ni saa nne na nusu asubuhi. Doreen alisikia sauti ya Bi Carolina ikimwita. Akatii wito na kumfuata Bi Carolina.
"Abee mama" aliitikia kwa heshima.
"Umeoga?"
"Bado"
"Kaoge unywe chai."
"Sawa mama"
Doreen alitoka sebuleni pale na kwenda bafuni kuoga. Alipomaliza alipaka mafuta na kuvaa tena nguo alizokuwa amevaa kabla ya kuoga kisha akaenda sebuleni. Akamkuta Bi Carolina akiwa amekaa huku akitazama televisheni.
"Mbona umevaa nguo chafu?"
"Sina zingine"
"OK.. Baadae tutaenda Mwanjelwa ukatafute nguo za kuvaa.. Sasa hivi nenda ukanywe chai.." Alisema Bi Carolina.
"Sawa mama.. Vipi kuhusu Dada Pamela?" Aliuliza Doreen.
"Atakuja si muda mrefu.. Ameniambia yupo njiani. Baada ya kumwambia hivyo ghafla mlango ukagongwa . Akaingia msichana mmoja mrefu kiasi, mweupe, matiti yenye ukubwa kiasi, kiuno chembamba kama sindano na makalio makubwa kama milima miwili iliyopangana vyema. Wote walishtuka kidogo.
"Ah Pamela kumbr ulikuwa jirani tu.. Tumekuongelea sasa hivi hapa.."
"Sikuwa mbali"
"Karibu sana" alisema Bi Carolina wakati huo Pamela alikuwa akiketi sofani na kuweka pembeni mkoba wake. Kwa muda wote huo Doreen alikuwa akimtazama Pamela katika maeneo ya kifuani.
"Shkamoo Dada Pamela" alisalimia Doreen
"Marhaba hujambo? Wewe ndo Doreen?"
"Ndio.." Aliitikia Doreen huku akimgeukia mama Pamela "kumbe una mtoto mzuri namna hii?" Alisema.
Bi Carolina na Pamela walicheka tu.
"Huyu ndo mwanangu mpenzi... Yuko peke yake kama Tanzanite..." Alisema Mama Pamela huku akicheka.
Doreen aliwaacha wakiendelea na mazungumzo kisha yeye akaenda chumba cha kulia chakula (dinning). Moyoni mwake alifurahi sana kwani kwa uzuri aliokuwa nao Pamela titi lake lilifaa sana kwa kazi ya Doreen.