Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Tanzania, Josephat Gwajima, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, kusikiliza kesi inayomkabili ya kutoa lugha ya matusi na kukutwa na silaha.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeahirisha kesi ya kutoa lugha ya matusi na kukutwa na silaha zinazomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Tanzania, Josephat Gwajima, kutokana na hakimu anayesikiliza shauri hilo kutokuwapo.
Kesi hiyo iliahirishwa leo na Hakimu Mkazi Magreth Bankika, ambaye alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Septemba 2, mwaka huu.
Askofu Gwjima alikuwapo mahakamani wakati kesi hiyo ikiahirishwa, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu iliporipotiwa kuwa ni mgonjwa.
Askofu Gwajima alifika mahakamani hapo saa 2:00 asubuhi akiongozana na walinzi pamoja na wafuasi wake.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, aliieleza mahakama kuwa shauri hilo limetajwa kwa ajili ya kusikilizwa na shahidi mmoja alikuwapo, lakini wamepata taarifa kuwa hakimu anayesikiliza shauri hilo hayupo, hivyo kuiomba mahakama kupangiwa tarehe nyingine.
Hakimu Bankika aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 2, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.
Katika kesi hiyo ambayo Askofu Gwajima anatetewa na Wakili Peter Kibatala, anadaiwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe, jijini Dar es Salaam, alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Policarp Kardinali Pengo, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Hivi karibuni Askofu Gwajima akiwa nje ya nchi, Jeshi la Polisi lilitangaza kumsaka kwa ajili ya kumhoji kutokana na mahubiri aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu kanisani kwake Ubungo.
Katika mahubiri hayo yaliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, askofu huyo alisikikika akiukosoa utendaji kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete na kumtaka Rais John Magufuli kumchukulia hatua kutokana na mabaya aliyoyafanya katika utawala wake.
Alipojea nchini alikamatwa na polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa kadhaa na kuachiwa.