SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 3 Agosti 2016

T media news

Kauli ya Serikali Kuhusu NGOs zinazohamasisha ushoga



WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wananchi na wadau kutoa taarifa, iwapo kuna mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) zinazojihusisha na kuhamasisha vitendo vya ushoga nchini ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.

Agizo hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Msajili wa NGOs, Marcel Katemba. Alisema kuwa siku za hivi karibuni, kumekuwepo na tuhuma za kuwepo kwa baadhi NGOs kujihusisha na kuhamasisha vitendo vya ushoga nchini.

Alisema ni vyema jamii ikatambua kuwa NGOs zinasajiliwa kwa lengo la kutekeleza majukumu yanayokubalika kisheria na kwamba vitendo vya kuhamasisha ushoga si majukumu halali yanayopaswa kutekelezwa.

“Tunazitaka NGOs kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya usajili wao na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria kwani kinyume na hayo hatua zitachukuliwa,”alisema Katemba na kusisitiza kuwa vitendo vya ushoga havikubaliki nchini kwani ni kinyume na mila, desturi na sheria za nchi.

Alisema katika kudhibiti uwepo wa vitendo hivyo, wadau na umma kwa ujumla wanapaswa kutoa taarifa zitakazowezesha kuthibitisha tuhuma hizo ili hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.

Katemba alisema taifa lina mila, desturi na sheria za nchi ambazo imekuwa ikizisimamia na kuzitekeleza na kuhamasishwa kwa vitendo hivyo kunakwenda kinyume na misingi, ambayo kwa namna moja vinaweza kuathiri kizazi kwa kizazi.

Alisema ni wakati sasa kwa kila NGO kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kama ilivyosajiliwa, kuongeza ushiriki wake kwa kutoa michango yao katika kuleta maendeleo kwa jamii.

Alisema taratibu za usajili wa NGOS chini ya sheria mashirika yasiyo ya kiserikali namba 24 ya mwaka 2002, yameimarishwa vyema na kila shirika linalokuwa limepata usajili ni muhimu kutekeleza yale yaliyokusudiwa ili kuepuka taifa kuingia katika vitendo visivyostahili.