Na Baraka Mbolembole
KIPAJI kikubwa cha uimbaji cha Ray C na Chid Benz kimekwamia katika matumizi ya madawa ya kulevya ‘Janga hatarishi zaidi kwa vijana hivi sasa.’ Kuna picha imeendelea kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, sijui kama ni Haji Mwinyi mlinzi wa kushoto wa timu ya Taifa ya Zanzibar, pia Taifa Stars na klabu bingwa ya Tanzania Bara.
Kimuonekano, kiumbile kuna tofauti kubwa na Haji Mwinyi ambaye wengi tunamfahamu kama mlinzi bora namba 3 Tanzania. Kama ni picha hii ni ya Haji kwa kweli nimeumizwa sana na pengine nimebaki njia panda kuamini ama kutoamiani kinachomtokea kijana huyo mdogo mwenye kipaji kikubwa cha soka.
Kuna siku nilioneshwa ‘live’ golikipa wa zamani wa Yanga, Noel Pompi jinsi alivyo hivi sasa unaweza kuumia mara nyingi zaidi ya hali ya sasa ya Mwinyi. Kiukweli nawalaumu sana viongozi wa Yanga kwa maana wamekuwa karibu na Hajji lakini hawaonekani kushtushwa na mabadiliko makubwa ya mchezaji huyo-kiumuonekano.
Kuna wakati iliandikwa habari ya Haji Mwinyi kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya-si ya kuongeza nguvu mwilini.
Lakini nakumbuka hata katika website hii iliwahi kuandikwa habari ya wazazi wake kukana huku wakisisitiza kwenda mahakamani kushtaki. Sijui iliishia wapi, lakini miezi michache mbele hivi sasa mwonekano wa Mwinyi unatia shaka na pengine huyu anaweza kuwa mchezaji wa kwanza mkubwa akionekana kuathiriwa na matumizi ya madawa ya kulevya.
Najiuliza, Yanga haina madaktari? Inachezaje michuano ya CAF ikiwa na wachezaji ambao labda wanatumia madawa ya kulevya?
Kiwango cha Haji katika game dhidi ya MO Bejaia kilikuwa ni cha chini na akaishia kulambwa kadi nyekundu katika mchezo wao wa kwanza wa Caf Confederation Cup 2016 hatua ya makundi mwezi Juni lakini mabadiliko aliyonayo sasa yanaumiza, yanasikitisha na najiuliza tu, inakuwaje timu kubwa kama Yanga inashindwa kuwapima wachezaji wao itakuwaje kwa klabu ndogo ambako ndiko wanakotokea kina Haji Mwinyi?
Kuna watu wengi wamewahi kushinda vita ya matumizi ya madawa ya kulevya. Mafano mdogo ni gwiji wa tungo na uimbaji ambaye amewahi kuwa mshauri wa raia wa Ivory Coast miaka ya nyuma.
Licha ya sifa nzuri katika tungo za mashairi, Alpha Blondy ni mmoja kati ya vijana wa kiafrika ambaye alilazimika kupigania maisha yake kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya…
Wakati fulani, serikali ya Ufaransa ilimrudisha kinguvu nchini mwao Ivory Coast baada ya kuwa ‘mteja’ wa kutupwa.
Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abdijan, Alpha alionekana kushindwa kutembea mwenyewe hivyo akasaidiwa na watu wawili. Ilikuwa ni mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Kama ni kweli Haji Mwinyi ni mtumiaji wa madawa ya kulevya ni wakati sahihi wa Yanga kumsaidia na imani yangu atarejea na kuwa mlinzi bora wa kushoto Tanzania.