Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitangaza mkakati wa chama hicho kufanikisha mikutano na maandamano ya walichokiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), huku jeshi la polisi nao wakijiandaa kukabiliana nao.
Mbowe aliitaja mikakati hiyo ikiwamo kamati za kuhamasisha Ukuta ambapo aliyekuwa mgombea urais kupitia Ukawa Edward Lowassa amepangiwa Mbeya, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji atakuwa Mwanza, Makamu Mwenyekiti Profesa Abdallah Safari atakuwa Tabora huku Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere Marando wakipangiwa Dar es Salaam.
Alisema yeye (Mbowe) ataongoza Kanda ya Kaskazini wakati Profesa Mwesiga Baregu amepewa jukumu la kufafanua Ukuta kwa taasisi za kimataifa, viongozi wa dini na wastaafu.
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu na mawakili 12 wao watajifungia Dar es Salaam kufungua kesi 21 kutetea mikutano.
Lakini, Jeshi la Polisi limesema litatoa taarifa rasmi baadaye huku CCM wakisisitiza msimamo wao wa kupinga maandamano hayo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema jeshi hilo litatoa taarifa siku chache zijazo. “Tutawaita na tutazungumza, naomba tujaribu tu kuvuta subira,”alijibu kwa ufupi msemaji huyo wa polisi.
Hata hivyo kikosi cha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika mikoa mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam na Kilimanjaro walionekana wakifanya mazoezi wakiwa na silaha na magari ya maji ya kuwasha kwa siku tofauti.
CCM watoa ushauri
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema licha ya chama kuzungumza mara kadhaa, wanatarajia kutoa tamko kwa lengo la kuwaeleza Watanzania tahadhari juu ya mchezo unaojaribiwa na Chadema.
Sendeka alisema viongozi wa dini na makundi mbalimbali yameshauri juu ya mipango yao, lakini hawataki kusikia.
“Jambo hilo limezungumzwa mara nyingi sana, viongozi wa dini wameshasema, watu wenye mapenzi na nchi yao wakishauri waache huo mchezo wao ambao sidhani kama watafanikiwa, kwa hivyo tunatarajia kutoa tamko letu siku yoyote kuanzia kesho (leo),”alisema.
Mbowe na safu yake
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini jana katika Hoteli ya Coridol Springs jijini hapa, Mbowe alisema chama hicho kimejipanga kufanya mikutano na maandamano ya amani nchi nzima Septemba Mosi ili kutetea utawala wa sheria na Katiba.
Mbowe alisema Rais Magufuli aliapa kuilinda Katiba, Wabunge waliapa kuilinda Katiba, madiwani waliapa kuilinda Katiba ili nchi iongozwe katika misingi ya sheria na utawala bora.
Alisema haiwezekani nchi kuongozwa kwa matamko ambayo yanakiuka katiba na Chadema kama chama kikuu cha upinzani kina wajibu wa kuishauri na kuikosoa serikali na hawawezi kukaa kimya.
Alisema matamko ya Rais kuwa hakuna ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa vyama vingine na kuacha chama chake kufanya mikutano na pia kuzuia mikutano hadi mwaka 2020 haikubaliki.
“Sisi tunataka nchi iongozwe kwa kufuata sheria na siyo matakwa ya viongozi ambayo yanakinzana na sheria na Katiba ya nchi,” alisema Mbowe.
Alisema wanafanya mikutano na maandamano kama sehemu ya kueleza malalamiko yao, hasa kutokana na kauli za viongozi ambazo zinakiuka sheria.
Mbowe alisema vyama vyote vikiamua kukaa kimya na kuacha mambo yaliyotokea Zanzibar, yaliyotokea Dodoma na yanayotokea sasa kutokana na kauli za viongozi, ni wazi nchi haitakuwa salama.
“Tukiamua sote kujifanya wanafiki kusema hewala nchi haitakuwa salama itazaa taifa la watu wenye hofu na ndiyo sababu tumeamua kamati kuu kuanzia sasa kufanya kazi kila siku kuisaidia sekretarieti,” alisema.
Mbowe alisema kutokana na unyeti wa Ukuta, Kamati Kuu ya Chadema imeunda kamati ndogo tano, ambazo zitasaidia kufikiwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuhusisha taasisi na vyombo vingine.
Alisema pia kuna kamati ya maandalizi ya Ukuta ambayo tayari imeanza kazi ya kufafanua maamuzi ya kamati kuu, ambayo sasa imesambaa katika kanda zote kutoa elimu kwa viongozi wa Chadema.
“Katika kanda zote nchi nzima viongozi watakwenda kuzungumza na wanachama wa kada zote na kuwaelimisha kwanini Kamati Kuu imefikia maamuzi ya kuanzisha Ukuta kabla ya kushiriki mikutano na maandamano Septemba Mosi,” alisema