Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kubadilisha mfumo wa uvunaji wa vitatlu vya miti kwenye mashamba ya Serikali ili kuweka uwazi kwenye biashara hiyo na kuipatia zaidi Serikali mapato.
Mhe. Majaliwa alisema hayo jana kwenye Mkutano na Viongozi pamoja na Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kisenga uliopo Kijitonayama Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Mhe. Majaliwa alisema kuwa utaratibu uliokuwa ukitumika hapo awali wa kuuza miti kwenye mashamba ya Serikali kwa njia ya vibali hauna tija kwakuwa umekuwa ukiikosesha Serikali mapato na kuwanufaisha wafanyabiashara wachache.
“Utaratibu wa sasa wa kutumia vibali unatuletea migongano ndani ya Wizara na kuikosesha Serikali mapato, hivyo ni lazima tuubadilishe” Aliongeza Majaliwa.
Aliuagiza Uongozi wa Wizara kufanya marekebisho kwenye utaratibu huo na kuweka utaratibu wa mnada ili kuweka uwazi zaidi na kuondoa manung’uniko kwenye biashara hiyo. “vibali visitishwe, mnada uanze kama inavyofanyika kwenye mitiki” Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Hivi karibuni Mhe. Majaliwa alisitisha utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti kwenye mashamba matano yanayomilikiwa na Serikali kutokana na kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa aliagiza mabadiliko ya haraka katika vizuizi vya ukaguzi wa Maliasili ambavyo amesema vimekuwa havina tija na kuagiza baadhi yake vifutwe kabisa. Miongoni vya vizuizi alivyoagiza vifutwe ni Kibaha Stendi, Kimanzichana na Mbagala, pia aliagiza kuimarishwa kwa kituo cha Vikindu, Kibiti na Vigwaza.
Mhe. Majaliwa aliwaagiza wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Tamisemi kwa ajili ya kuweka mfumo mzuri wa kuhifadhi na kuvuna mazao ya misitu yaliyopo katika Halmashauri na kutenga Misitu ya Asili tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo kumekuwepo muingiliano katika kutekeleza majukumu hayo jambo linalopelekea uharibifu wa misitu.
Hapo awali Mhe. Majaliwa alieleza lengo kuu la Mkutano huo kuwa ni katika utaratibu wake wa kawaida aliojiwekea wa kutembelea Wizara na kuzungumza na watumishi kwa ajili kukumbushana majukumu yao, kuangalia changamoto mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.
Aliwaasa watumishi wa Wizara ya Maliasili kuwa wazalendo, waadilifu, waaminifu na kuongeza uwajibikaji ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kuwahudumia vizuri wananchi.
“Ninyi ni watu muhimu sana katika utoaji wa huduma kwa wananchi, tekelezeni majukumu yenu kwa uadilifu wa hali ya juu. Kamilisheni malengo yenu kulingana na mpangokazi wenu mliojiwekea”Alisema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisisitiza watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa wanalinda misitu kule iliko na sio kusubiri katika vituo na kukamata rasilimali zake ambazo zimevunwa isivyo halali na kuzitoza faini, kinyume chake rasilimali hizo zilipiwe kihalali kabla ya kuvunwa. Aliahidi pia kuisuka upya Idara ya Misitu.