SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 15 Julai 2016

T media news

Watumishi Watatu Wasimamishwa Kazi Jeshi La Polisi



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya malipo hewa, yaani kulipa posho ya chakula (Ration Allowance) kwa watu ambao sio askari

Hatua hii ni mwendelezo wa uchunguzi wa tuhuma za kufanya malipo hewa ya kiasi cha sh. 305,820,000/= zilizopelekea kusimamishwa kazi kwa Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Bw.Frank Charles Msaki wiki iliyopita.

Kwa Mamlaka ya Katibu Mkuu chini ya Kanuni ya 35(2)(b) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 zikisomwa pamoja na Kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Kuanzia tarehe 13 Julai, 2016, amewasimamisha kazi wafuatao: Bw. Damian Aloys Bupamba ambaye ni Mhasibu Daraja la II na Bi, Ida Dennis Moyo Mhasibu Daraja la I kwa makosa ya kufanya malipo ya posho ya chakula kwa watu wasiostahili kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.

Aidha kwa Mamlaka ya Katibu Mkuu chini ya Kifungu cha 7(4) cha Sheria Na.8 ya Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza ya Mwaka 1990 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 2015 kikisomwa pamoja na Kanuni C.23(1)(b) ya Kanuni za Utumishi wa Jeshi la Polisi za mwaka 1995 zilizorekebishwa mwaka 2013, kuanzia tarehe 13 Julai, 2016, amemsimamisha kazi Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Milambo Mwita Milambo kwa makosa ya kufanya malipo ya posho ya chakula kwa watu wasiostahili kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.

Watumishi wote watatu wamehusika kufanya malipo haya jambo ambalo ni kinyume na Kanuni F.9 ya Kanuni za Utumishi wa Jeshi la Polisi za mwaka 1995 kama zilizovyorekebishwa mwaka 2013.

Katibu Mkuu amewasimamisha wahusika hawa ili kupisha Uchunguzi wa tuhuma dhidi yao unaofanyika kufuatia Uchunguzi Maalamu wa Mkaguzi wa Ndani wa Jeshi la Polisi uliobaini makosa ya malipo hewa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi