TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema inatarajia kukamilisha mchakato wa katiba inayopendekezwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, aliyama hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kutembelea banda la tume hiyo katika Maonyesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema katiba inayopendekezwa itaweka maoni ya wananchi juu ya mapendekezo ya tume huru ya uchaguzi wanayoitaka na hivyo uchaguzo ujao utakuwa katika mfumo huo.
Jaji Lubuva alisema ili kufanyika kwa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, ni lazima kwanza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na NEC zikutane ili kufanya marekebisho ya sheria ya taifa ya uchaguzi.
"Ni matumaini yetu na tungependa sana kuona kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ujao 2020, tuwe tumeshapata katiba mpya ambayo itatupa muongozo wa uchaguzi mkuu huo," alisema.
Alisema ili kupata tume ya uchaguzi ambayo itakuwa huru, itatokana na kupatikana kwa katiba mpya ambayo mchakato wake unatarajiwa kumalizikia kwenye kura ya maoni.
Hata hiuvyo, Jaji Lubuva alisema tume iliyopo ni huru kwa sababu haiingiliwi na mtu yoyote isipokuwa kinachosabisha isionekane huru ni mfumo wake wa kuteuliwa kwa makamishna nane na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama.
"Tume iliyopo ni huru na haki kwa sababu kazi zetu haziingiliwi na yeyote na hata uchaguzi tulioufanya mwaka jana ulikuwa huru na haki isipokuwa watu walishaaminishwa tume siyo huru, "alisema Jaji Lubuva na kuongeza:
“Wanachokitaka Watanzania ni kuona wanakuwa na tume huru ya maandishi pamoja na isiyoingiliwa na yeyote. Nchi yetu ina tume huru na haki, ni tofauti na nchi nyingine ambazo zipo kwenye maandishi tu lakini si huru.”
Juzi Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura utafanyika mwaka wa fedha wa 2017/18.
Alisema kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa inaweza kufanyika kabla au baada ya uboreshaji wa daftari hilo.
Hata hivyo, alisema daftari hilo litaanza kiboreshwa mara baada ya sheria ya uchaguzi kufanyiwa marekebisho na kupitishwa.