Mtunzi: Enea Faidy
....DORICE alimtazama malkia yule kwa woga huku fimbo ile ya dhahabu ikiwa kifuani mwake. Alihisi kifo chake kipo njiani lakini akajipa moyo wa imani kuwa hawezi kufa kwani hakutenda kosa lolote. Malkia Yule alicheka kicheko kikali cha kutisha.
"Dorice wewe ni mchawi sio?" Alisema Malkia yule huku akiwa na sura ya kutisha sana.
"Mimi sio mchawi!" Alijibu Dorice kwa kutetemeka.
"Mbona ulipovamiwa na chatu pale njiani uliongea maneno ya kichawi?"
"Ndio niliyaongea lakini mimi so mchawi, maneno hayo nilifundishwa na babu yangu ambaye ni mganga!" Dorice alishikwa na woga kupita kiasi.
"Hahah Dorice... Kuwa mkweli?"
"Kweli kabisa.. Mimi si mchawi.. Tafadhali naomba mniruhusu niende!" Alisema Dorice huku akilia.
"Unaenda wapi?"
"Naenda Singida kwa babu yangu!"
Aliomba Dorice akiwa amepiga magoti huku akilia kwa hofu.
"Huwezi kwenda Dorice... Sahau kuhusu kuondoka hapa!" Alisema malkia yule kisha akamwamrisha mlinzi wake amwondoe pale Dorice ampeleke sehemu nyingine.
Mlinzi alitii agizo la malkia akamtoa Dorice pale na kumpeleka eneo lingine.
Kilikuwa kama chumba kidogo chenye mwanga hafifu lakini kilikuwa na mapambo mengi sana ya dhahabu. Kilipendeza sana na kilivutia macho kupita kiasi, Dorice alibaki anashangaa.Aliingizwa chumbani mle bila kuambiwa kitu chochote na mlango ukafungwa. Akabaki peke yake.
Hofu ilimzidia sana alitetemeka kama MTU aliyekumbwa na baridi Kali sana, hakupata fursa ya kutazama kitu chochote ndani ya chumba kile akabaki ameinama huku akilia. Alijuta kutoroka shule kwaajili ya Doreen, aliona heri angebaki tu kuliko kuchukuliwa na viumbe wale wa ajabu.
Ghafla akiwa katika dimbwi zito la mawazo alishtuliwa na sauti nzito ya kiume ikimwita jina lake."Dorice" Dorice alishtuka sana kwani alipoingizwa mle hakukuwa na mtu yeyote wala hakusikia mlango ukifunguliwa.Aliinua kichwa na kumtazama aliyemwita.
"Usiogope Dorice.. Naitwa Mansoor, ni mtoto wa Malkia.." Alijitambulisha mwanaume Huyo mwenye sura nzuri ajabu, alinukia marashi mazuri sana yasioisha hamu kuyanusa. Dorice alishangazwa na uzuri wa kiumbe yule mwenye umbo tofauti na viumbe wengine aliowaona kwenye eneo lile. Kwa haraka alimkadiria kuwa na umri wa miaka kama 21 au 22.
"Dorice! Nimeshangazwa sana na uzuri wako uliojaaliwa.. Ama kweli umeumbika! Karibu kwenye himaya yetu!" Alisema kijana yule aliyejitambulisha kwa jina la Mansoor huku akitabasamu na kumpa mkono Dorice. Dorice alibaki ameduwaa kwa mshangao.