Na Athumani Adam
Paul Pogba kijana wa Kifaransa mwenye asili ya Guinea, ni mmoja wa viungo ambao wamekamilika kwenye ulimwengu soka. Pogba ana kila kitu, anafunga, anafanya ‘tackling’ za uhakika bila kusahau soka lake la kutumia nguvu na akili nyingi uwanjani. Wataliano kule jijini Turin kwenye klabu yake ya Juventus wamembatiza jina la Polpo (pweza) sababu ya miguu yake mirefu wengine wanasema ni Patrick Viera mpya.
Pogba anahusika na tetesi za kurudi Manchester United baada ya kuondoka mwaka 2012 kuelekea Juventus ya Italia baada ya kumgomea babu Sir Alex Ferguson kusaini mkataba mpya. Kuna kila dalili ya kurudi Old Trafford sababu hawa ni aina ya wachezaji ambao meneja wa Manchester united, Jose Mourinho ana wazimia. Siku zote Mourihno anapenda kuwa na watu wagumu kwenye timu zake anazofundisha.
Alipokuwa Chelsea aliwahi kuwa na Michael wawili wenye mioyo migumu, Essien na Ballack. Intermilan alikuwa na Cambiasso na Wesley Sneijder alipoenda Madrid alikuwa na Xabi Alonso.
Kupitia kwa wakala wa Pogba, Mino Riola ambaye tayari amefanya biashara na Man United msimu huu baada ya kumpeleka mteja wake Zlatan Ibrahimovic kule Old Trafford amesema, alitaka kumuuza Pogba kwenye Klabu ya Chelsea msimu ulioisha. Kwa lugha nyingine Mourinho alimtaka Pogba tangu akiwa Chelsea msimu uliopita. Ukweli wa hili anajua Riola Mwenyewe.
Kutokana na mwenendo huu, Man United kuna uwezekano wa kutoa pesa nyingi zipatazo Euro Milioni 100 ili kumnasa Pogba. Hiyo ndio bei yake kwa mujibu wa Juventus. Pogba hakuwa na thamani hiyo misimu mitatu iliyopita. Lakini hata kama ikitokea Pogba akauzwa kwa kiasi pungufu ya hicho kuelekea Man United, bado United itakuwa imeingia gharama kwasababu ya dharau zao
Sir Alex Ferguson alifanya dharau wakati akiwa kocha wa Man United. Ferguson hakumpa Pogba nafasi ya kutosha kucheza kwenye timu ya wakubwa. Muda mwingi alitumikia kikosi cha academy au kikosi cha pili, tangu alipojiunga na Man United akitokea Le Havre mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka kumi na saba.
Babu Ferguson mara chache alimpa Pogba nafasi kwenye timu ya wakubwa japokuwa takwimu za Pogba kwenye timu za vijana pale United zilikuwa za kuvutia. Kutokana na dharau hizi Pogba akasaini mkataba na Juventus kimyakimya hatimae babu Ferguson akawa amechelewa.
Hli ni kosa ambalo hata kipindi kile Sir Alex Ferguson aliwahi kukili linaweza kuja kuigharimu Man United pale aliposema “I mean if we hold Pogba back, what’s going to happen? He’s going to leave” akimaanishaa kama wataendelea kutomtumia Pogba, kitachotokea ni yeye kuondoka.
Pogba angekuwa bado yupo United kama angesaini mkataba angalau wa miaka minne kutokana na umri wake, lakini kosa la Sir Alex Ferguson kutompa nafasi ya kucheza sasa linawachanganya mabosi wa United wakifikiria jinsi gani watarudisha lulu ambayo Sir Alex Ferguson aliipoteza kirahisi.
Sijui kama Man United watafanikiwa kumrudisha Pogba, kwa sababu hawapo pekee yao kwenye mbio hizi, wapo pamoja na wababe wa fitna za usajili barani Ulaya Real Madrid. Madrid ambayo ina kiungo mmoja wa kweli mwenye uwezo wa kukaba bwana mdogo Casemiro bila shaka nadhani pia Zinedine Zidane anamtamani Pogba kweli kweli.