SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 20 Julai 2016

T media news

Nay wa Mitego: Rapper Mtukutu Anayewaumiza Kichwa BASATA


Nay wa Mitego ni kama yule mtoto mtundu sana kwenye familia ambaye amepinda kiasi cha kutojali wazazi watasema nini. Ni yule mtoto ambaye wazazi wamemkanya kwa kila style lakini ni kama maneno yanapita sikio la kushoto na kutokea la kulia – hajali.

Kwa walioanza kumfuatilia Nay tangu anaanza kujulikana kwa nyimbo kama Kitafamika, wanaelewa kuwa muziki anaofanya Nay ndiyo wa hivyo siku zote. Ni rapper anayezungumza mada ngumu kuzungumzwa na wengine. Ni rapper anayezungumza ukweli unaochoma na wakati mwingine sentensi ambazo kwa mtu wa kawaida si rahisi kuzitamka.

Ni rapper ambaye kwa wenzie wakati mwingine amekuwa akigeuka kuwa mwiba wenye sumu. Amewahi kumchana hata P-Funk Majani, producer wa kwanza kabisa kurekodi naye na aliyemtengeneza kwa kiasi fulani kuwa hapo alipo kwa kumfananisha na Ja Rule.

“Naikumbuka zamani kipindi cha Majani, nyimbo kali redioni zilitoka kwa Majani, ngoma kali top ten alitengeneza Majani, lakini leo Majani kapuni, Majani gizani, Majani maji shingoni, oyaa Majani kunani? Eti Majani ni nani?” anarap Nay kwenye Itafahamika.

Aliwahi kumchana pia rapper ambaye kwa wengi hawawezi kuthubutu hata kufungua kimya kumkosoa – Chidi Benz kwa kumtania kwa kitendo chake cha kutoboa pua huku akimuelezea kuwa ‘pengine sio riziki.’

Pamoja na kuwa mwiba kwa wasanii wenzake waliopotea, Nay alisababisha povu kubwa kwa wasanii wa bongo movies kwa alichokisema kwenye wimbo wake ‘Nasema Nao.’ “Makahaba wenye viwango wapo bongo movie, bongo movie ka danguro poleni Ray na JB,” anachana Nay.

Anafahamika pia kwa kuchana hata wanasiasa. Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Zitto Kabwe ni miongoni mwa wahanga wa mistari yake controversial.

Malalamiko kwenye nyimbo zake kutoka kwa mastaa wenzake yalikuwa mengi mno kiasi cha kuwafanya BASATA waanze kumwangalia kwa jicho la ukaribu na kumuonya hapa na pale. Nay hakuwa na sifa nzuri kwenye baraza hilo kiasi ambacho aligeuka kuwa mfano wa msanii anayeimba vitu visivyo na maadili.

Wakati mwingine mistari yake huwa mizito kiasi cha kuzikuna hata sharubu za vyombo vya dola. “Wanangu nyongeni ganja msiogope polisi,” anarap kwenye Salam Zao.

Uvumilivu wa BASATA ulifika kikomo baada ya rapper huyo kutoa wimbo wake ‘Shika Adabu Yako’ mwaka huu na kama kawaida kuning’inia shingoni kwa mastaa wenzake kwa maneno ya kejeli. Wahanga wa wimbo huo walikuwa ni pamoja Shilole, Snura, Ray, Wema Sepetu, Ommy Dimpoz, Diva, Shettah na wengine.
Cha kuchekesha zaidi ni kuwa Nay aliwachana pia BASATA kwenye wimbo huo.

“Hizi ni taarifa zangu na ziwafikie BASATA, nyie ni kuku au bata msumeno usiokata, kazi kufungia nyimbo mnajua shida tunazopata? Hamjui wajibu wenu mngekuwa watoto tungeshawachapa,” anarap.

Pengine Nay alivuka kiwango cha uvumilivu wa baraza hilo na ndio maana liliufungia. Hakutikitiswa na hilo, badala yake aliachia video yake ambayo licha ya kutochezwa kwenye TV, iligeukuwa miongoni mwa video zake zenye views nyingi zaidi kwenye mtandao wa Youtube.

Amani ilirejea alipoachia Nasaka Pesa lakini imekuja kuvurugika tena hivi karibuni alipoachia wimbo wake mpya, Pale Kati. Kama jina lenyewe linavyoonekana kuwa controversial, ndivyo ilivyokuwa pia kwenye picha za kuupromote zilizosambaa mtandaoni.

Kwenye moja ya picha Nay anaonekana akiwa amekaa katikati ya wasichana wawili walioweka migongo lakini makalio yao yakiwa matupu. Tayari wimbo huo umeshafungiwa na BASATA na wiki hii aliitwa kwenda kujieleza. Bado amekuwa akidai kuwa wimbo huo utakuwa na video takriban nne bila kujali kama baraza hilo limeufungia.

Hadi sasa Nay amebaki kuwa msanii pekee mwenye kesi nyingi zaidi na baraza hilo kiasi cha watu kuanza kumtabiria adhabu kubwa zaidi siku za usoni kama hatobadili mienendo yake.

Nafahamu kuwa adhabu kama hizo zimekuwa na athari ndogo kwa rapper huyo kwakuwa bado ameendelea kuwa na show nyingi zinazomlipa, lakini siku za usoni zinaweza kugeuka kuwa jinamizi litakalomsumbua.

Labda ni muda sasa Nay akakubali kuwa imetoshaa kuwa na nyimbo controversial na kuanza kufanya nyimbo tofauti bila kuwatengenezea wasanii wenzake picha mbaya kwa anachokisema kuwahusu. Kwamba labda siku moja akaja kumchana asiyechanika. Amewahi kukiri pia kupata vitisho vingi kutoka kwa aliowachana bila kusahau kuwa amepoteza marafiki zake wengi wa zamani.

Japo amewahi kupata endorsement na Airtel, pengine licha ya ushawishi alionao, skendo kama hizi za kufungiwa nyimbo zake zinaweza kumkosesha ulaji mkubwa zaidi kutoka kwa makampuni ambayo yangependa kufanya naye kazi lakini yakaogopeshwa na CV yake mbaya.

Chanzo:Bongo5