Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) amesema amewasilisha barua kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai akitaka Naibu Spika aondolewe madarakani kwa kukiuka kanuni za uendeshaji Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari Msigwa amesema kwamba muswada wa fedha uliopitishwa na Bungen lililomalizika ulipitishwa kinyume na taratibu.
''Muswada wa fedha wa mwaka 2016 wenye namba 9 ulichapwa tarehe tarehe 03 Juni 2016 na kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza na kwa utaratibu wa bunge ukaenda kufanyiwa kazi na kamati ya bajeti na katika katika majadiliano na wadau ikaonekana muswada huo ulihitaji marekebisho makubwa hivyo serikali ilitakiwa kuleta jedwali la marekebisho jambo ambalo halikufuatwa''- Amesema Msigwa.
Msigwa ameongeza kuwa ''Naibu Spika amekiuka kanuni na namna muswada huu ulivyopitishwa hata wabunge wa CCM wengi hawakukubaliana nao ila yeye akaupitisha''
''Kwa mantiki hii nimemwandikia barua Spika wa Bunge kwa kutaka kumuondoa Naibu Spika Tulia Ackson Mwasasu kwa kushindwa kusimamia kanuni za bunge wakati wa kupitisha sheria ya fedha ya mwaka 2016'' amesema Msigwa.
Wabunge wa kambi ya upinzania katika bunge la 11 mkutano wa 3 uliomalizika walisusia vikao kwa zaidi ya wiki 3 wakitoka nje baada ya kudai kwamba Naibu Spika Dkt. Tulia Mwansasu anaendesha Bunge isivyo.
Hata hivyo Naibu Spika alisikika akisema anaendesha Bunge hilo kwa mujibu wa kanuni na kama wabunge hao wanatatizo na uendeshaji wake wa bunge watumie kanuni na si kususia vikao vya bunge.