SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 14 Julai 2016

T media news

DAKTARI FEKI MOROGORO MAPYA TENA YAIBUKA,MENGI YAELEZWA


Daktari feki, Zakaria Benjamin Migomba akiadhibiwa baada ya kukamatwa kabla ya kupelekwa kituoni.
MOROGORO: Mambo mapya yameibuka kufuatia kukamatwa kwa Zakaria Benjamin Migomba (35), akidaiwa kujifanya daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, baada ya kubainika kuwa wakati akipekuliwa na askari, alikutwa na Biblia.

Katika tukio ambalo mwandishi wetu alilishuhudia, Migomba alikutwa na kitabu hicho kitakatifu ambacho alikitumia kusoma kikiwa kwenye kibegi chake, kabla ya kunyang’anywa huku pia baadhi ya ndugu zake wakijitokeza na kutoa ushuhuda wa kushangaza.

 

Mdogo wa Migomba ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema ndugu yake ni mgonjwa wa akili na kwamba miaka michache iliyopita, aliwahi kupelekwa katika hospitali maalum ya wagonjwa wa akili ya Mirembe mkoani Dodoma, ambako alitibiwa na kupata nafuu, akaruhusiwa kurejea nyumbani kisha akaoa.


“Sisi tulikuwa tunamtafuta maana ametoweka nyumbani bila kujua alikoelekea, sasa tuliposikia kuna mtu amekamatwa hapa hospitalini, ndipo nilipokuja na bahati nzuri nimemkuta ni yeye. Inabidi tusikilizie kinachoendelea lakini kiukweli ‘braza’ akili yake kuna wakati haikai sawasawa,” alisema kijana huyo.


 

Naye mlinzi wa zamu aliyekuwepo siku ya tukio, Jackson Chacha, alipoulizwa mtu huyo alipitaje bila kujulikana, alisema tatizo ni kwamba hospitali hiyo haina uzio, hivyo mtu mwenye nia ovu anaweza kuingia kwa kupitia eneo lolote ambalo halina walinzi.

 

Migomba anayetajwa kuwa mkazi wa Tungi katika Manispaa ya Morogoro, alikamatwa Julai 10, mwaka huu baada ya nesi wa zamu katika chumba cha wagonjwa mahututi, kumshtukia alipoingia akiwa na koti linalotumiwa na madaktari. Kabla ya kuingia katika wodi hiyo, mtu huyo tayari alikuwa ameingia na kuzungumza na wagonjwa katika vyumba namba moja, tisa na saba.