SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 1 Mei 2016

T media news

Watu wenye ulemavu wa ngozi Malawi katika hatari ya kuangamizwa kikamilifu

Watu wenye ulemavu wa ngozi au albino nchini Malawi wanakabiliwa na hatari ya kuangamizwa kikamilifu kutokana na kuongezeka vitendo vya hujuma dhidi yao nchini humo.

Hayo yamedokezwa na mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu wa ngozi, au albino. Ikponwosa Ero ameonya kuwa machungu na vitisho vinavyowakabili albino nchini Malawi vinahatarisha uwepo wao iwapo hatua hazitachukuliwa.

Akizungumza baada ya ziara yake rasmi ya kwanza nchini Malawi Bi. Ero amesema albino katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika wanaishi kwa hofu kubwa, hawalali na hata hawawaamini wale wanaopaswa kuwalinda kutokana na familia kuhusika katika baadhi ya matukio ya wao kushambuliwa.

Bi. Ero amesema hali ni mbaya zaidi kwa kuwa tangu mwaka 2014 visa 65 vya mashambulizi dhidi ya albino viliripotiwa nchini Malawi vikiwemo visa viwili wakati wa ziara yake.

Amesema fikra potofu za matumizi ya viungo vya albino katika ushirikina na kwamba albino hawafariki dunia bali wanatoweka zinahatarisha zaidi maisha yao.

Pamoja na kupongeza mpango wa serikali wa mwaka 2015 wa kuwalinda albino, bado ametaka mafunzo zaidi yatolewe kwa polisi, waendesha mashtaka na mahakimu ili hukumu za kesi hizo ziendane na ukubwa wa tukio husika.

Mwaka jana Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, alielezea wasiwasi wake juu ya ongezeko la mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, albino.

Alisema nchini Tanzania, Malawi na Burundi albino wamekuwa wakitekwa nyara na kujeruhiwa na wengine kuuawa akisema watu watatu kati yao wamekumbwa na visa hivyo wiki iliyopita pekee.

Umoja wa Mataifa anataka nchi husika kuimarisha ulinzi kwa watu wote wenye ulemavu wa ngozi kwenye maeneo yote yenye mashambulizi na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wote, na kuhakikisha kwamba matibabu na huduma kwa wahanga na familia zao vinapatiwa kipaumbele.