Shirika la Kimataifa la Wahajiri IOM limesema hatima ya wahajiri zaidi ya 80 haijajulikana hadi sasa baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama katika pwani ya Libya kwenye bahari ya Mediterranean Ijumaa iliyopita.
Flavio Di Giacomo, msemaji wa IOM mjini Rome amesema watu 84 wametoweka na kwamba 26 pekee ndio walionusurika katika mkasa huo. Ameongeza kuwa, wakimbizi 1,400 waliokolewa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya boti zao kuzama na kwamba 237 miongoni mwao wamepelekwa katika kisiwa cha Lampedusa.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Kamisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa, wahajiri 41 tu kati ya 541 waliokuwa katika boti iliyozama karibu na mji wa Tobruk, ndio waliookoka na kwamba, wahajiri 500 walizama baharini.
Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa tukio hilo ndilo baya zaidi kuwahi kutokea baharini katika miaka ya hivi karibuni. Wahajiri hao kutoka nchi za Kiafika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri walikuwa wakitoroshwa kutoka katika mji wa Tobruk kuelekea Ulaya.
Wakimbizi karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee na wengine karibu 700 wamefariki dunia kwa kuzama baharini.