Na Athumani Adam
Mwaka 1990 mchezaji raia wa ubeligiji, Jean Marc Bosman ambaye alikuwa anachezea timu iliyokuwa daraja la kwanza nchini kwao iitwayo RFC Liege alishindwa kuhamia nchini Ufaransa kwenye klabu ya Dunkerque.
Japokuwa Bosman alikuwa tayari amemaliza mkataba na klabu yake, lakini alishindwa kwenda Ufaransa sababu ikiwa ni Dunkerque kushindwa kufikia makubaliano na klabu ya awali ambayo Bozman alikuwa anacheza.
Kipindi hicho cha miaka ya 90 na kabla ya hapo, timu ambayo inamtaka mchezaji hata kama amemaliza mkataba ililazimika kulipa ada ya usajili kwa timu ile ambayo mchezaji amemaliza nayo mkataba. Basi Bosman akaamua kutafuta haki yake, akaenda zake mahakama ya Ulaya kule nchini Luxembourg kufungua kesi kuhusu jambo hili.
Kitu ambacho Bosman alikuwa anapigania wakati ule ilikuwa ni kuona mchezaji endapo anamaliza mkataba aweze kuhamia timu nyingine akiwa huru yaani timu anayotoka isipate chochote kwa kuwa haina mamlaka tena na mchezaji husika.
Ilipofika mwaka 1995, mahakama ikatoa umauzi wa kesi ile baina ya Bosman dhidi ya klabu yale RFC Liege. Bosman akashinda kesi ile na kuanzia hapo mchezaji anakuwa huru kuhaima timu nyingine endapo akimaliza mkataba bila timu yake ya awali kupata kitu.
Sheria hii imekuwa maarufu sana kwenye soka inatambuliwa kama sheria ya Bosman yani ‘Bosman rule’.
Kutokana na sheria hii vilabu vingi Ulaya vina jitahidi kuwapatia wachezaji wao mahiri mikataba mipya pindi mkataba yao inapobaki mwaka mmoja kabla ya mikataba kuisha
Hebu kumbuka lile sakata la De Gea pale mkataba ulipobaki mwaka mmoja kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwezi August mwaka uliopita. Kumbuka nguvu ambazo zilitumiwa na kocha wa United, Luis Van Gaal kumshawishi kipa wake asiondoke.
Lengo la vilabu ni moja tu, hawataki mchezaji aondoke huru hivyo kitendo cha kuongeza mkataba kitasaidia kuiingizia klabu pesa kipindi ambacho akitakiwa na klabu nyingine hususan kwenye karne hii ambayo mpira ni biashara.
Hata pale ikitokea mchezaji akiondoka huru basi mara nyingi huwa hayupo tena kwenye mipango ya muda mrefu na klabu. Kama itavyotokea kwa naodha wa Chelsea, John Terry mwsihoni mwa msimu huu.
Nimeanza na stori ya Bosman kutokana na mambo ambayo hutokea kila mwishoni mwa msimu wa ligi hapa nchini. Nimesoma kupitia gazeti moja la michezo hapa nchini habari ya wachezaji nane wa Stand United kumaliza mikataba yao na sasa wanaelekea kuondoka wakiwa huru.
Kwenye kundi hilo yupo mfungaji bora wa klabu hiyo, Elius Maguli, Haruna Chanongo, Rajab Zahir, Abuu Ubwa na wachezaji wengine wanne. Tupo kwenye dunia ya peke yetu ambayo mfungaji bora anaondoka huru au mchezaji mahiri mwenye umri chini ya miaka 25 kama Chanongo anakwenda zake bure.
Mazoea ya viongozi wetu kuanza mazungumzo ya mkataba hadi mkataba wa mchezaji unapofikia mwisho kabisa ni sababu ya kupoteza wachezaji hata kama wapo kwenye mipango ya muda mrefu na timu hizo.
Kwenye hili Stand wametangulia tu, muda si mrefu tutasikia vilabu kadhaa vikipoteza nyota wake kwa staili hii. Kwa hapa nyumbani suala hili kwa sasa ni kama limezoeleka wala hakuna anayejali. Leo limeanza Stand United, kesho litaenda sehemu nyingine Yanga, Simba, Azam, Mwadui.
Stand na wengineo kila mwisho wa msimu wanakubali maamuzi ya Luxembourg kirahisi, maamuzi ambayo yalimpa Bosman ushindi huku vilabu vyao vikipoteza pesa ya usajili. Jambo ambalo lisinge tokea kama mchezaji angekuwa na mkataba.
Viongozi wa vilabu vyetu hawana muda wa kujifunza kwa wenzetu kuhusu suala la mikataba. Siku zote viongozi makini hulinda mikataba ya wachezaji wao nyota. Chelsea wamefanya kwa Hazard, Madrid wakafanya kwa Ronald, Barcelona wamefanya kwa Messi
Viongozi wetu hawana tabia ya kuandaa mazingira ya mikataba mipya pindi ile ya awali unapofikia japo katikati. Viongozi wetu wapo tayari kupoteza mchezaji kirahisi kwasababu wanajua watatoa fedha za mfukoni kuziba pengo la mchezaji.
Wakati Ronaldo amepewa mkataba mpya siku chache zilizopita japokuwa mkataba wake ulibaki mwaka mmoja, kwetu huku mabosi ndiyo kwanza hawana habari na wachezaji wao nyota, wapo tayari kuona wanaondoka wakiwa huru kupitia sheria ya Bosman.