SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 1 Mei 2016

T media news

AZAM FC ‘ITAWAPOTEZA’ ZAIDI SIMBA SC, YOTE HAYA YAMEANZIA HAPA… (Sehemu ya mwisho)

Na Baraka Mbolembole

SIMBA SC itakuwaje masikini wakati ni taasisi kubwa na ya kale sana iliyokuwapo hata kabla ya Tanganyika kupata uhuru (1961), kisha kuzaliwa kwa Tanzania (1964)?

Ngoja nikupe mfano mmoja hai, Kabla ya serikali ya awamu ya tano chini ya rais John Pombe Magufuli raia wengi wa Tanzania waliaminishwa kwamba nchi hii ni masikini sana na haiwezi kujiendesha kiuchumi bila kutegemea misaada ya mataifa makubwa duniani.

Jambo ambalo kwa mtu aliyesoma na kuelewa vizuri somo la maarifa daima alikuwa akipinga. Muda mfupi wa serikali ya Magufuli madarakani nchi imejikusanyia mapato mengi baada ya kuwekwa kwa mkakati wa kudhibiti mapato ya serikali yaliyokuwa yakipotea-ama kwa walafi wachache, ama kwa wakwepaji wa kodi.

Rais Magufuli anasifiwa na kila mtu hivi sasa kutokana na uwezo wake wa kuwabaini ‘wahujumu uchumi’ na kuwachukulia maamuzi. Ameyaonesha mataifa makubwa kwamba Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe kiuchumi kwa kutegemea rasilimali zake, na vyanzo muhimu vya mapato.

Ukiwa kama rais au kiongozi mwenye mamlaka ni lazima uwe na maamuzi magumu ambayo wakati mwingine yanaweza kumuathiri hata mzazi wako, rafiki yako wa karibu ama washirika walioshikamana na wewe wakati ukipambana kufika mahala hapo ulipo kiutawala.

Utawala labda ni kipaji kama inavyosemekana, ama ni taaluma ambayo muhusika anapaswa kuisomea. Wapo wanaoamini katika kipaji kwanza cha mtu kisha taaluma. Vyote vinategemea, na ili mtu uwe kiongozi makini unapaswa kuwa na vyote hivi (kipaji na taaluma).

Katika soka, walio wengi wanaamini kwamba mwanasoka aliyepita anafaa zaidi kuwa kiongozi wa klabu ya soka kutokana na uzoefu wake wa vitendo wakati wa uchezaji wake. Labda si kweli kwa maana hata kiongozi aliyepita kama mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alipata kuwa mchezaji wa timu hiyo miaka ya nyuma lakini kiutawala alishindwa vibaya.

Pia kuna kundi lingine la mashabiki wanaamini mtu yeyote makini kiutawala anaweza kuwa kiongozi mzuri katika soka licha ya kutokuwahi kuwa mchezaji wa mchezo huu. Labda ni kweli kwa kuwa miaka mitatu ya Yusuph Manji kama mwenyekiti wa klabu ya Yanga SC ameweza kujipambanua kama mmoja wa viongozi wazuri waliopita katika klabu hiyo.

Najua wanachama wa klabu hawana mamlaka ya kumtoa Poppe katika timu yao, lakini hasira zao dhidi ya mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili na ile ya ujenzi wa uwanja wa klabu-Bunju Complex wakati timu yao ilipochapwa 1-0 na Toto Africans ya Mwanza wiki iliyopita ni ishara ya kumchoka mtu huyo ‘anayejitapa kila mara kwamba yeye ndiye anayeisaidia Simba’ bila kutoa ufananuzi anaisaidia kutoka katika vyanzo gani vya mapato.

Simba kama ingekuwa na mtu kama Michael Wambura na namna ushindani ulivyo kutoka kwa klabu za Yanga na Azam ni wazi Simba ingekuwa katika mwelekeo unaoonekana na si kama huu wa miaka miwili ya kwanza ya utawala wa Aveva ambao bado timu haieleweki uelekeo wao ni wapi.

Katika sehemu ya nne ya makala nilipata comment ya mmoja wa viongozi wa zamani wa timu ya Simba, C.Magori, yeye alisema kwamba sipaswi kuwabeza Friends of Simba kwa maana tangu mwaka 2000 ndiyo wamekuwa wakiisaidia timu hiyo kujiendesha kiuchumi.

Hakuna mwana Simba asiyekubaliana na hili na hata mimi wakati nakua niliamini hivyo lakini katika ufahamu na uelewa wangu wa sasa ni uongo uliotukuka kusema Friends of Simba ndiyo kila kitu kwa miaka hii 16. Hawa ni watu wanaoiyumbisha klabu vile wanavyotaka, wanainyong’onyesha kiuchumi na kuidumaza ili waonekane ni muhimu kila mwaka. Hakuna mkubwa kuliko Simba Sports Club na Friends of Simba si taasisi eti ambayo inaweza kuisaidia Simba kiuchumi kwa miaka 16 mfululizo.

Mimi nawatazama kama watu wa kwanza waliididimiza timu kiuchumi na Aveva akithubutu kuendelea kuwashikilia nakwambieni Simba itakaa misimu 6 mfulizo bila taji hadi mwaka 2018 itakampopata mtu mwenye mtazamo kama wa Wambura (Rejea sehemu ya tatu ya makala haya).

Ningependa kuona misimu minne ya Aveva ikiwa ya taabu na timu yake isishinde VPL ili baadhi ya wanachama wasiomakini wakati wa upigaji kura wapate kujifunza. Ndiyo hao sasa wanalazimisha MO auziwe timu.

Ni vyema sasa timu hiyo ikajisimamisha yenyewe kiuchumi. Simba haina bahati na hawa kina Dewji. MO si suluhisho. Nafikiri Azam FC itachochea utambi kwa Aveva kuvunja kamati yake ya usajili kama njia ya kwanza ya kumtoa Poppe katika kamati ya usajili. Simba ‘itachanwa chanwa’ katika game ya ligidhidi ya Azam FC.

Matatizo yote ya Simba yalianzishwa na ‘hat-trick’ ya John Bocco katika pambano la Robo fainali Kagame Cup, 2012. Timu iliyokuwa imesajiliwa vibaya, tena kwa gharama kubwa ilivyunjwa mwezi mmoja baadaye. Azam itaipoteza zaidi Simba na kuweka ushawishi kwa Poppe kujiuzulu.

ASANTENI kwa kuwa pamoja mwanzo hadi mwisho. Ilikuwa ni hoja tu, ila katika hoja kweli huja.