Baraka Mbolembole
Wakati Yanga SC ikiangalia jinsi gani ya kuifunga Esperanca ya Angola na kuitoa katika ‘play off’ ya michuano ya Shirikisho Afrika siku ya Jumamosi katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mlinzi wa kushoto wa timu hiyo, Oscar Joshua anasema kwamba hawatashawishika kwa namna yoyote ile kuamini mtazamo wa baadhi ya watu kwamba Waangola hao si timu kali.
“Hii si nafasi ya wazi kwetu, na hatufikirii kabisa kwamba wapinzani wetu wajao katika michuano ya CAF ni timu rahisi. Hatuwazii hivyo, tunavyojua sisi (Yanga) Esperanca ni timu ngumu na lazima tujiandae kushinda na wala hatupo tayari kupokea mawazo kuwa hiyo ni timu rahisi. Hatushawishiki kwa hilo hata kidogo”, anasema Oscar wakati nilipofanya naye mahojiano marefu akiwa mkoani Shinyanga ambako aliisaidia timu yake kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji wao Stand United katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara siku ya Jumanne.
Yanga itacheza mchezo wa kwanza nyumbani, na hawatapaswa kwa namna yoyote kusubiri kuona jinsi Esperanca watakavyocheza katika uwanja wa Taifa kama msaada wa kuwasaidia kujua jinsi ya kucheza mchezo wa marejeano nchini Angola.
Huu ni muda mzuri kwao wa kutulia na kuwasoma Esperanca kwa undani zaidi ili kuendelea kucheza vizuri kama wanavyofanya katika michuano ya ndani ya nchi. Katika mbio zao za kufuzu kwa hatua ya makundi ndani ya miaka hii mitatu ya CAF, bila shaka Yanga wako katika nafasi muhimu zaidi kuanzia Jumamosi hii kwa maana wanakutana na timu isiyo na uzoefu mkubwa zaidi yao.
“Mechi zetu mbili za Shirikisho zina umuhimu mkubwa sana, kutengeneza historia ya klabu na sisi wachezaji itakuwa ni mafanikio yetu mengine makubwa. Pia itakuwa ni kama zawadi kwa mashabiki wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono kila wakati.” anasema Oscar aliyekutana na upinzani mkali katika beki 3 mbele ya Mwinyi Hajji msimu huu.
“Katika misimu yangu mitano niliyocheza hapa (Yanga) tulikuwa na timu nzuri, lakini kikosi hiki cha sasa ni kikali sana. Kwanza ushindani wa namba umekuwa mzuri kwa maana umemsaidia kila mchezaji kulinda kiwango chake na kuchangia kuwepo kwa ulingano mkubwa wa kiwango cha anayecheza na mchezaji asiyecheza mechi mara kwa mara. Timu hii ya sasa magoli yanafungwa kwa wingi sana tofauti na misimu iliyopita”, anasema Oscar aliyecheza game 15 za mashindano yote hadi sasa (mechi kumi za VPL, 3 za FA Cup na nyingine 2 za klabu bingwa Afrika.
“Mechi 15 kwangu hazitoshi lakini hakuna budi ndiyo hizo zimetokea na bado mapambano yanaendelea. Kwa kweli ushindani miaka yote unakuwapo na kikubwa ukiwa na subira na uvumilivu ukiwa pia una muomba Mungu utafanya vizuri kwenye kazi yako. ”
“Kutokucheza kwangu kwa mechi za nyuma naamini ulikuwa wakati wangu wa kutafakari nini nifanye na pia ilikuwa sehemu ya mapumziko kwani msimu uliopita nilicheza mechi nyingi sana za ligi na michuano ya CAF hata timu za Taifa.”