Umoja wa Mataifa umepinga maonyesho ya picha za kipropaganda za utawala wa Kizayuni wa Israel katika makao makuu ya umoja huo mjini New York.
Imedokezwa kuwa maonyesho hayo ya Israel yalikuwa yafanyike leo Jumatatu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo utawala wa Tel Aviv ulikuwa umepanga kuonyesha picha za kutetea sera zake za kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Balozi wa utawala haramu wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon amekasirishwa sana na hatua ya kupigwa marufuku maonyesho hayo na kusema jambo hilo linahatarisha uwepo wa Israel.
Utawala wa Kizayuni ulipanga kuonyesha picha ambazo zingearifisha mji wa Quds eti kuwa ni mji mkuu wa Israel. Wapalestina wanasisitiza kuwa Quds ni mji mkuu wa dola huru la Palestina.
Kwingineko Harakati ya Kimatiafa ya Kususia Israel BDS imeitaja kuwa ni ushindi mkubwa hatua ya kupigwa marufuku uonyeshaji wa filamu ya Kizayuni ya 'Mwili wa Tatu' katika maonyesho ya filamu za haki za binadmau huko Seoul Korea Kusini.