SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 9 Aprili 2016

T media news

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Aeleza matumaini yake Kutokomeza malaria Katika Bara la Afrika




RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema, ana imani kwamba kupitia ushirikiano uliopo baina ya serikali mbalimbali barani Afrika, mashirika ya kimataifa, makampuni binafsi na kila mtu katika nafasi yake, ugonjwa wa malaria unaweza kumalizwa kabisa.

Kikwete alionesha matumaini hayo juzi wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa jitihada za kuutokomeza ugonjwa wa malaria (Malaria no more) zilizoanzishwa na Ray Chambers akishirikiana na Peter Chernin.

Katika hafla hiyo, Kikwete alitunukiwa tuzo ijulikanayo kama White House Summit Awards ikiwa ni kutambua uongozi wake, kujitoa kwake na kubwa zaidi kusimamia uanzishwaji wa muungano wa viongozi wa Afrika dhidi ya malaria (ALMA), muungano ambao hadi sasa una viongozi 49.

Wengine waliotunukiwa tuzo hiyo ni Ray Chambers na Sumitomo Chemical. Akijibu swali la nini anadhani kimechangia katika kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria, Kikwete alisema zipo sababu kadhaa, lakini kubwa ni utashi wa kisiasa wa kusimamia na kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Akawaeleza wageni zaidi ya 250 walioalikwa wakiwa ni wawakilishi wa makapuni na mashirika mbalimbali yanayochangia juhudi za kuukabili ugonjwa wa malaria kwamba, upatikanaji na usambazaji wa dawa sahihi za kutibu ugonjwa wa malaria, utengenezaji, usambazaji na matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu na unyunyiziaji wa dawa za kuua mazalia ya mbu ni mambo ya msingi ambayo yamechangia katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.