SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 5 Machi 2016

T media news

Ukiukwaji haki za binadamu Misri walaaniwa

Vikosi vya usalama vya Misri vimelaumiwa kwa kukiuka haki za binadamu kutokana na kutekeleza vitendo vya utesaji na mauaji ya kiholela wakati wa kukabiliana na wapinzani.Ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Egyptian Initiative for Personal Rights umesema serikali ya Misri inayopata himaya ya kijeshi imenyamazia kimya ukatili wa vikosi vya usalama vya humo.Mtafiti wa shirika hilo la haki za binadamu, Sherif Mohy Eldeen amesema ukiukwaji wa haki za binadamu ni njia inayotumiwa na vikosi vya usalama dhidi ya wapinzani. Ameongeza kuwa maafisa wa polisi ya Misri wanakiuka sheria bila kujali huku baadhi ya maafisa wa serikali wakihimiza ukatili huo wa polisi.Mwezi Januari Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch liliikosoa serikali ya Misri kwa kutumia mkono wa chuma kuwakandamiza wapinzani.Watawala wa Misri wanawatazama wapinzani kama wahaini hususan viongozi harakati ya Ikhwanul Muslimin pamoja na wafuasi wao. Watu wasiopungua 1,400 wameripotiwa kuuawa nchini Misri katika ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama vya serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na jeshi tangu Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, alipopinduliwa na jeshi mwezi Julai 2013 katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Rais wa sasa wa nchi hiyo Abdul Fattah el-Sisi.