SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 12 Machi 2016

T media news

UGONJWA WA KISUKARI UNAVYOATHIRI MWILI


Haina mashaka yoyote kuwa vyakula vya nafaka vinanoga!  Au wewe unasemaje kuhusu wali mweupe, pilau, biriani?  Na bado hapo hujagusia chipsi, chapati, kitumbua, andazi, bagia na ugali wa sembe.

Sina shaka yoyote ile kuhusu ubaya wa kubugia kwa wingi vyakula vya nafaka.  Tukumbuke kwamba sukari, yule adui namba moja wa afya, chimbuko lake ni nafaka.  Naamini wengi wetu tunajua kuwa sukari ni miongoni mwa vyakula vikuu vinavyosababisha mfuro (uvimbe) na hii ni moja ya vyanzo vikuu vya mwili inayosababisha kisukari.

Kisukari ni nini?
Sukari kinachoingia katika mzunguko wa damu inatokana na vyakula tunavyokula.  Inapokuwepo kwa wingi katika mzunguko huo, mwili kutoa taarifa kwa kongosho ili kufanya kazi ya ziada kuzalisha kiwango kikubwa cha kichocheo kinachojulikana kama insulin ili kuondoa sukari kwenye damu na kuipeleka kwenye seli ili itumike kutengeneza nishati.

Hali hii ikijirudiarudia mara kwa mara, kongosho huchoka na kuanza kufanya kazi chini ya kiwango au wakati mwingine vipokezi vya sukari katika seli (receptors) hushindwa kuendana na kasi ya kuletewa sukari kwa ajili ya matumizi ya seli, hivyo huishia kuikataa.

Hali hii, kitaalamu hujulikana kama insulin resistance, au pingamizi dhidi ya insulin kwa tafsiri isiyo rasmi.  Kuna baadhi ya nyakati, vyote hutokea kwa wakati mmoja, yaani kongosho linafanya kazi chini ya kiwango na pia mgonjwa anakabiliwa na pingamizi dhidi ya insulin.  Hapo mgonjwa husumbuliwa na tatizo la sukari.

Hivi karibuni imebainika kuwa moja ya sababu kubwa sana zinazosababisha vipokezi vya seli kushindwa kupokea sukari inayoletwa ni kitu kinachoitwa mfuro (inflammation).  Mfuro ni uvimbe kama lengelenge hivi.  Mfano wa mfuro ni pale unapojikwaa au kujigonga usoni na mwili ukaumuka na kutengeneza nundu.

Vichocheo vya kusababisha mfuro kwenye seli viko vingi lakini baadhi ni vyakula tunavyokula kila siku.  Vyakula hivi ni pamoja na sukari na wanga iliyotokana na nafaka iliyochakatwa kwa kiwango kikubwa.

Chimbuko la nafaka kusababisha mfuro ni sukari aina ya fructose ambayo ama tayari ipo au inakuwa ni moja ya mazao wakati nafaka inachakatwa ndani ya miili.

Watafiti wanasema fructose huchochea seli za mwili kuchoma nishati iliyohifadhiwa kwa kasi ya kutisha na matokeo yake hukumbwa na matatizo ama mshtuko.

Mshtuko huo husababisha vina saba (DNA) katika hizi seli kusambaratika.  Watafiti hawa wanaongeza kuwa DNA iliyosambaratika hujiunda katika kemikali zinazojulikana kama purines, ambazo nazo huishia kujiunda kuwa tindikali ya urea, yaani uric acid.

Tindikali ya urea husababisha seli za mwili kukumbwa na mfuro ambao huharibu mifupa laini inayounganisha viungo vya mwili, husababisha mishipa ya damu kukumbwa na mkakamao wa kutokupanuka wala kusinyaa, kitendo ambacho husababisha matatizo ya mfumo wa mzunguko wa damu.

Kwa upande mwingine, glukozi au sukari nyingine inayopatikana kwa wingi kwenye nafaka au mezani, inaweza kuleta shida kwenye ini.  Inaweza ikasababisha unene uliopitiliza na inaweza kuchochea kisukari cha ukubwani na saratani.  Glukozi pia ni chanzo kikubwa sana cha mfuro ndani ya mwili!

Kwa mujibu wa tafiti, uchakataji wa glukozi huzalisha kemikali inayoitwa malonyl-coA hupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa mitochondria kudhibiti chembe chembe zilizobeba umeme hasi (high energy electrons) zinazotumika wakati wa uzalishaji wa nishati inayoitwa Adenosine Tri-phosphate (ATP), ambayo ni kwa ajili ya matumizi ya baadaye mwilini.  Mitochondria inaweza kuelezewa kama ni viwanda vya kuzalisha nishati ndani ya seli.  Huu umeme husababisha kuzaliwa kwa kiwango kikubwa cha chembe zilizobeba umeme chanya zinazoitwa free radicals.  Chembe hizi zina uwezo wa kubadilisha umbo na utendaji kazi wa vinasaba kwenye seli (DNA mutations) na kuharibu vimeng’enya mbalimbali ndani ya mwili.  Tafiti zimebaini kuwa baadhi yetu, miili huchakata ngano bila madhara ukilinganisha na wengine.  Watu wa aina hii husemekana wana mifumo ya ujenzi na uvunjifu wa kemikali ambazo zinaendana na vyakula vya wanga hasa itokanayo na nafaka.  Njia pekee ya kujua kama wewe ni miongoni mwa waliomo katika kundi hili au siyo ni kwa njia ya kipimo cha kutambua mfumo wa ujenzi na uvunjifu wa kemikali mwilini (metabolic typing test).