SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 4 Machi 2016

T media news

Kinachosababisha macho kutoona




Macho ni moja ya milango mitano ya fahamu. Kazi yake ni kuhakikisha binadamu anaona mazingira yanayomzunguka. Bila macho huwa ni vigumu kwa binadamu kuyatawala mazingira yake.

Ili kuweza kutawala vyema mazingira yake binadamu anahitaji macho ambayo yanaona vizuri na mfumo wa fahamu ambao unaweza kutafsiri mwanga wa taswira ambao unafikishwa kwenye ubongo kupitia macho.

Kwenye makala yetu leo hii tunaangalia changamoto mbalimbali ambazo zinasababisha macho kushindwa kuona vizuri na matokeo yake kusababisha taswira yenye kasoro kwa ajili ya kutafsiriwa na ubongo. Macho kushindwa kuona vizuri husababisha mwanga wa taswira unaopelekwa kwenye ubongo kupitia mshipa maalumu wa fahamu wa macho kuwa na upungufu.

Ingawa tatizo linaweza kuwa kwenye jicho moja mara nyingi madhara yake kwenye tafsiri inayofanywa na ubongo huhusisha macho yote.

Dalili ni kama vile kuona taswira mbili tofauti kutokana na jicho moja kuona vizuri na jingine kutoona vizuri, kushindwa kuona au kupata matatizo ya kuona kwenye eneo lenye mwanga mdogo.

Dalili nyingine ni kushindwa kuona wigo mpana zaidi ya eneo ambalo jicho limedhamiria kutazama na kuona ukungu na kushindwa kutambua kitu vizuri. Kwa kawaida kushindwa kuona vizuri huwa ni tatizo la macho lakini mara nyingine hali hii hutokea pamoja na dalili nyingine. Inapotokea tatizo la kuona vizuri likaambatana na dalili nyingine mara nyingi huashiria tatizo kubwa linalohitaji kufanyiwa vipimo na kupatiwa ufumbuzi.

Dalili mbaya zinazoambatana na tatizo la kuona vizuri ni kama vile kichwa kuuma sana, kushindwa kuongea vizuri kunakoambatana na kushindwa kuona vizuri na kukosa nguvu mwilini; hususani kupoteza nguvu kwenye upande mmoja wa mwili

Dalili nyingine mbaya ni upande mmoja wa uso kushindwa kufanya kazi kabisa, maumivu makali ya macho na tatizo la kushindwa kuona vizuri kadiri siku zinavyoenda.

Kuna sababu nyingi zinazosababisha mtu kushindwa kuona vizuri. Baadhi ya sababu ni kama vile mtoto wa jicho, mkwaruzo au uambukizo kwenye jicho, kama vile korinea na retina, mbele wa jicho, maradhi yatokanayo na umri, kipanda uso, kisukari, kiharusi na majeraha.

Tatizo hili kwa watu wengi huanza taratibu na ili kuweza kujua chanzo cha tatizo ni muhimu sana kwa daktari kuuliza historia ya tatizo na kufanya vipimo vya kawaida vya macho na mwili kabla ya kumshauri mgonjwa kufanya vipimo vikubwa zaidi vya macho. Historia ya maradhi mengine ni muhimu pia kwa daktari kuifahamu kwa kuwa inaweza kuwa sababu ya tatizo a kutoona vizuri.

Vipimo vitakavyofanyika sio tu vitahusisha macho lakini pia inaweza kuhusisha mifumo mingine ya mwili kama damu na kadhalika.

Matibabu ya matatizo ya macho hutegemea matokeo ya vipimo vya chanzo vya tatizo. Chanzo cha tatizo hutoa mwanga wa kama tatizo linatibika ama halitibiki. Kwa wengi wenye tatizo la kutoona vizuri matibabu ya tatizo huhusisha tiba ya chanzo halisi.

Matibabu hulenga kutatua chanzo cha tatizo na kutatua tatizo la macho. Kinga ya matatizo mengi ya macho huhusisha ulinzi wa macho kwa kuyakinga na madhara ya moja kwa moja.

Kutokana na sababu za tatizo kuhusisha mifumo mingine pia ni vyema tutambue kuwa kulinda afya kwa ujumla kunaweza kusaidia kukinga macho na tatizo hili.

Vaa miwani ya kuzuia mwanga mkali, kula mlo wenye virutubisho muhimu kwa macho na nawa mikono kabla ya kugusa macho kwa vidole.