Matukio ya wajawazito kupoteza watoto kwa madai ya uzembe wa wahudumu wa afya yameendelea kuugubika Mkoa wa Mwanza baada ya mkazi wa Nyarawambo wilayani Sengerema Tatu Muhangwa, kujifungua na mtoto wake kufariki kwa kukosa huduma.
Mama mzazi wa Tatu, Vumilia Nailon alisema mjukuu wake alifariki baada ya wahudumu wa afya katika Zahanati ya Ngoma ‘B’ iliyopo Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema, kuchelewa kumhudumia.
Mhudumu wa afya aliyekuwa zamu, Helena Mulwisha alisema alishindwa kumhudumia mjamzito huyo kutokana na kubaini kuwa mtoto alikuwa kakaa vibaya tumboni na kuwashauri kumpeleka hospitali ya wilaya kwa msaada zaidi.
Nailon alisema: “Nilimfikisha mgonjwa wangu zahanati juzi, saa kumi na moja alfajiri, lakini hadi saa tatu hakuwa amepatiwa huduma yoyote hadi alipojifungua mwenyewe bila msaada na mtoto kufariki.
“Mmoja wa wahudumu wa afya aliyekuwapo alishindwa kumhudumia baada ya kugundua mtoto amekaa vibaya tumboni na yeye hana utaalamu wa kumsaidia.”
Alisema Mulwisha aliwashauri kumpeleka mgonjwa hospitali ya wilaya kwa sababu wauguzi na madaktari walikuwa wakihudhuria semina.
“Baada ya kukosa gari ya kumuwaisha hospitali, tuliamua kutembea kwa miguu umbali wa kilomita mbili, lakini hatukufika baada ya magonjwa wangu kujifungulia njia kwa msaada wa wasamaria wema na mtoto kufariki,” alisema Vumilia.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk Henry Nyamete alisema ofisi yake inachunguza tukio hilo na kwamba itachukua hatua za kinidhamu dhidi ya mhudumu wa afya aliyekuwa zamu siku hiyo kwa kushindwa kuwajibika kwa kuita gari la wagonjwa ili kumuwahisha mjamzito huyo hospitali kwa matibabu zaidi.