SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 29 Machi 2016

T media news

EDWARD Lowassa Afunguka: Niacheni Kwanza Jamani...

Ikiwa ni miezi minane tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuhamia CCM na kutua Chadema, jana alitoa sadaka yake ya kumshukuru Mungu kwa mambo mengi aliyomtendea na anayoendelea kumtendea. 

Hata hivyo, wakati Watanzania wengi wakisubiri kauli ya Lowassa aliyegombea urais 2015, kwa tiketi cha Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, akiwa katika Kanisa Kuu la Kilutheri la Azania Front jijini Dar es Salaam jana alisema: "Niacheni kwanza".

Lowassa ambaye alishiriki ibada hiyo maalum  ya kutoa sadaka ya shukrani yake na familia, alipoulizwa juu ya maoni yake kuhusiana na uchaguzi huo, alisema “Tungeje kidogo kitakachoendelea huko. Niache kwanza nitaongea.”

Aidha, aliwapongeza viongozi wa dini kwa kuhuribi amani nchini na kwamba ndiyo tunu pekee inayotakiwa kulindwa kwa kiasi kikubwa.

“Nawatakia sherehe njema wabarikiwe katika sherehe hii ya Pasaka, tuendelee kuhubiri amani ndiyo tuzo pekee tuliyonayo. 

Nawashukuru viongozi wa dini kufanya wajibu wao, ni wajibu wetu nasi kufanya wajibu wetu kwa hayo tuliyohubiriwa,” alisema.

Juzi wakati wa ibada ya Pasaka katika kanisa hilo, kulikuwa na tetesi za Lowassa kuwapo na wangekutana uso kwa uso kwa mara ya kwanza na Rais Dk. John Magufuli, ambaye alisali kanisani hapo kwa kushtukiza.

Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, aliwatangazia waumini kuwa Lowassa na familia yake watatoa sadaka maalum ya shukrani kwa Mungu kutokana na mambo mbalimbali aliyowatendea na anayoendelea kuwatendea.

Kama Lowassa angeshiriki ibada ya juzi, ingekuwa ni mara ya kwanza kwa wawili hao ambao walikuwa wagombea wanaochuana kwa karibu zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kukutana na kukaa katika eneo moja.

Katika uchaguzi huo Okotoba 25, mwaka jana, Dk. Magufuli aliibuka mshindi kwa zaidi ya kura milioni nane dhidi ya Lowassa aliyepata kura zaidi ya milioni sita.

Hata hivyo, Lowasaa amekuwa akipinga matokeo hayo akidai kuwa alishinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 64.

Duru za kisiasa zinaeleza kuwa Lowassa angeweza kugusia hali ya kisiasa Zanzibar na hasa uchaguzi wa marudio uliofanyika bila wapinzani wakuu wa CCM, ambao ni CUF sambamba na utendaji kazi wa Serikali ya Magufuli, lakini alikwepa.

Pia Lowassa ni msharika wa Azania Front, lakini katika ibada iliyohudhuriwa na Rais hakuwapo.

Akitoa salamu za Pasaka, Rais aliwaomba Watanzania kumuombea kwa kuwa kazi ya uongozi aliyonayo siyo ndogo na kuacha kubaguana kwa vyama, dini na makabila ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii kuiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Katika ibada ya jana, Lowassa aliambatana na familia yake, watoto na wakwe zake akiwamo Sioi Sumari, huku viongozi wa Ukawa wakiwakilishwa na James Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Magaeuzi.

Wengine waliohudhuria ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya wa Ilala, Charles Kuyeko na Meya wa Kinondoni, Jacob Boniface, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji.
Watu maarufu waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Malecela, Balozi Emmanuel Ole Naiko na Askofu wa Dayosisi ya Morogoro, Jacob Ole Mameo.

Katika ibada hiyo, ilitarajiwa kuwa Lowassa angezungumza, lakini Askofu Malasusa alimkaribisha Askofu Mameo kuzungumza kwa niaba ya wageni wote ambaye alimpongeza kiongozi huyo kwa kuwa mtoaji.

“Nimekuja kumsindikiza kaka yangu Lowassa kutoa sadaka yake ya shukurani ya pekee maana ni jambo la busara na hekima kumtolea Mungu, nilimkaribisha wakati natoa shukrani yangu ya pekee Ubungo kanisani, nakumbuka maneno aliyoniambia,” alisema na kuongeza:

“Baba Askofu Mameo umekuwa mfano wa viongozi wa juu wa Kanisa wanaokumbuka kutoa shukrani kanisani maana Wakristo raia tumezoea kutoa na ninyi (viongozi wa kanisa) hamtoi, nami nasema ni bahati ya pekee kuwa na watu wacha Mungu wanaokumbuka kumrudishia Mungu shukrani zao kwa mambo aliyowatendea.Tunapoona watu wa aina hiyo, ni lazima tuwaunge mkono na Mungu ndivyo anavyotaka, tunafanyiwa mambo mengi sana na Mungu.”

“Namshukuru sana kaka yangu Lowassa anamtolea Mungu mara kwa mara na anatendewa mambo mengi na Mungu na ndiyo maana hadi sasa yupo na Mungu, anapenda watu wanaotoa shukrani. Katika vitabu vya Ijinili, Yesu aliwaponya watu 10, mmoja ndiye alirudi kushukuru, sote tuna sababu ya kumshukuru Mungu kwani tunatendewa mengi sana,” alisisitiza.

“Lowassa tutaendelea kukuunga mkono, umetendewa mambo mengi sana, kutoa  siyo jambo la kuiga ni la moyoni na kama siyo la kuiga utaendelea kulitenda kila mara siyo kwa kuambiwa,” alisisitiza.

SAFARI YA LOWASSA MILIMA NA MABONDE 
Machi 20, mwaka 2014, CCM ilitangaza kuwafungia kwa miezi 17 makada wake sita waliodaiwa kuanza kampeni za urais kabla ya muda ulioruhusiwa na chama na walifunguliwa Mei 22, mwaka jana.

Chama hicho kilisema kitafanya tathmini kama walikiuka kanuni za adhabu hiyo na iwapo ingebainika wangechukuliwa hatua zaidi.

Baada ya kufunguliwa na kabla ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake (wakati huo) kupeperusha bendera ya chama hicho, makundi mbalimbali yalikwenda nyumbani kwake mjini Dodoma kumshawishi kuchukua fomu ya urais na ilipoelezwa kuwa makundi hayo yaliandaliwa naye, alisema hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono.

Lowassa alikutana na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali nchini Mei 27, mwaka jana na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ikiwamo kueleza safari ya matumani.

Lowassa akiwa ameambatana na makada mbalimbali wa chama hicho katika Uwanja wa Shekhe Amri Abeid jijini Arusha Mei 30, mwaka jana na kutangaza kuanza safari ya matumaini ambayo itatimiza ndoto za Watanzania kupata elimu bure, majisafi na salama na maendeleo kwa ujumla, kisha kutangaza rasmi nia ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM wakati huo.

Mafuriko ya Lowassa yaliteka jiji hilo na kuvunja rekodi ya mikutano iliyowahi kufanyika nchini huku kukiwa na viongozi maarufu kama kada wa zamani Kingunge Ngombale-Mwiru, wenyeviti wa CCM wa mikoa mbalimbali na waliowahi kuwa mawaziri na watumishi serikalini.

Lowassa alichukua fomu katika makao makuu ya CCM mjini Dodoma Juni 4, mwaka jana na kutembeza kuomba wadhamini kwenye mikoa yote nchini huku kukiwa na mafuriko ya watu na alirejesha Julai mosi, mwaka jana.

Hata hivyo, safari ya matumaini ya kiongozi huyo kwa CCM iliishia Julai 10, mwaka jana, baada ya kikao cha Kamati Kuu (CC) kukata jina lake na kupitisha jina la Dk. Magufuli, jambo lililozua taharuki na maandamano ya wafuasi wake katika mji wa Dodoma na viunga vyake kiasi cha polisi kuingilia kati kuwatawanya.

Julai 27, mwaka jana, Lowassa alijiunga rasmi Chadema na kukabidhiwa kadi ya uanachama wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho na baadaye alitangaza kupeperusha bendera ya Ukawa katika uchaguzi huo.

Baada ya kuhama, makada wengine akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, walimfuata na alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chadema kuwania nafasi hiyo.

Agosti 10, mwaka jana, Lowassa alichukua fomu ya kuwania urais katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Nec ilipuliza kipenga cha kampeni Agosti 22, mwaka jana, Lowassa alifanya kampeni kwa gari na helkopta katika maeneo mbalimbali nchini, huku kukiwa na vita kali ikiwamo ya kueleza udhaifu wa afya yake na kutuhumiwa kwenye majukwaa ya kisiasa ya wapinzani wake wa karibu.

Oktoba 29, mwaka jana, Nec ilimtangaza Dk. Magufuli mshindi wa nafasi ya urais kwa kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 dhidi ya Lowassa aliyepata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97.

Baada ya matokeo hayo, Lowassa alikuwa kimya na licha ya kushawishiwa na makundi ya vijana kutoa tamko kali, hakufanya hivyo na kuwataka kuwa watulivu.

Kutokana na hali hiyo, Desemba 19, mwaka jana, Lowassa alitunukiwa tuzo ya amani na taasisi za kidini 1,200.