SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 5 Machi 2016

T media news

Bandari yajitetea matishari mabovu Tanga


Ufisadi ulioibuliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye bandari ya Tanga, bado unaitesa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo imetoa taarifa ndefu ya kujitetea huku ikikiri kwamba matishari hayo hayajafanya kazi tangu yanunuliwe.

Matishari hayo yaliyonunuliwa kwa Dola za Marekani 10,113,000 sawa na zaidi ya Sh. bilioni 21, hayajafanya kazi kwa miaka mitano licha ya kwamba muuzaji ameshalipwa asilimia 87 ya malipo yake.

Mamlaka hiyo imetoa taarifa kuelezea mchakato mzima wa ununuzi ulivyoanza mwaka 2011 hadi matishari hayo kufika katika bandari ya Tanga.

Kwa mujibu wa tarifa ya TPA, matishari hayo kwa mujibu wa mkataba wao na muuzaji yalipaswa kusafirishwa kwa njia ya kubebwa na meli lakini haikuwa hivyo.

Ilisema matishari hayo yalivutwa kutumia boti badala ya kubebwa na meli kama walivyokubaliana kwa madai kuwa matishari hayo yalikuwa makubwa mno kupakiwa kwenye meli.

Ilisema wakati yakiwa njiani kuja nchini, yalikumbana na dhoruba ya kimbunga kikali baharini na kusababisha boti iliyokuwa ikiyavuta kuzama na matishari hayo kugongana kisha kusukumwa na mawimbi hadi nchini Malaysia.

TPA ilisema ajali hiyo ilisababisha matishari hayo kupata hitilafu lakini kwasababu yalikuwa na bima, gharama za matengenezo zilibebwa na bima iliyokuwa imekatwa.

Ilisema baada ya matengenezo yalivutwa hadi bandari ya Tanga na yalipofanyiwa ukaguzi yalibainika kuwa na kasoro kadhaa zilizosababisha zisifanye kazi iliyokusudiwa kwa wakati huo.

“Yalikuwa na mifuniko ambayo ilibainika kuwa si rafiki katika shughuli za kupakia na kupakua na muuzaji alitakiwa kuyafanyia matengenezo kwa gharama zake mwenyewe,” ilisema taarifa ya TPA.

Aidha, TPA ilifafanua kuwa wakati matishari hayo yakifanyiwa majaribio kulikuwa na changamoto kadha kama vile ukubwa wa tishari kusababisha kreni za meli kushindwa kupanga mizigo vizuri.
Ilisema kulihitajika boti kubwa kwa ajili ya kuvuta matishari hayo na kwamba tayari mamlaka imeiagiza na inatarajiwa kufika nchini kuanzia Juni.

Mamlaka hiyo ilisema imemwagiza muuzaji wa matishari hayo kuyafanyia marekebisho na kuhakikisha yanakuwa katika hali ya kutumika na ndipo atakapolipwa malipo yake ya mwisho.

TPA ilisema kwenye taarifa yake kuwa bado inadaiwa Dola za Marekani milioni 1.4 (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 3) tu na muuzaji huyo.

Malaka hiyo imesema zitalipwa baada ya majaribio kufanyika na kubainika kuwa matishari hayo yanaweza kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mamlaka hiyo ilitoa zabuni ya kutengenezewa matishari matatu kwa mtu aitwaye John Achelis na kampuni ya Sohne Gmbh ambapo kila moja lilipaswa kuwa na ukubwa wa tani 3,500.