Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaka Umoja wa Afrika (AU) kuchukua hatua za makusudi ili kusimamisha umwagaji wa damu za raia wasio na hatia huko Sudan Kusini.Ripoti mpya ya Human Rights Watch imewataka viongozi wa AU kuanzisha koti maalumu za kusikiliza kesi za jinai zinazodaiwa kufanywa na maafisa usalama wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika hususan katika eneo la Western Equatoria.Bekele, Mkurugenzi wa shirika hilo barani Afrika amesisitiza udharura wa kuchukua hatua za haraka kusimamisha mapigano hayo, ambayo kwa sasa yameanza kuenea katika maeneo mengine haswa upande wa magharibi mwa nchi. Kadhalika Human Rights Watch imeutaka Umoja wa Mataifa kuwawekea vikwazo vya silaha wapiganaji wa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa Sudan Kusini.Hii ni katika hali ambayo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International (AI) limelituhumu jeshi la Sudan Kusini kwamba limefanya uhalifu wa kivita kwa kuwakosesha pumzi kwa makusudi makumi ya raia waliorundikwa katika kontena la kusafirisha bidhaa lililokuwa na joto kali, katika Jimbo la Unity Oktoba iliyopita. Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake za zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba amehusika na jaribio la kupindua serikali yake.