Uhabeshi ambayo hii leo inajulikana vyema kwa jina la Ethiopia ni nchi ambayo ni mashuhuri sana kwa Waislamu. Katika makala hii tumejaribu kadiri ya uwezo wetu kubainisha angaa kwa ufupi hali ya kihistoria, kijografia, kieneo kisiasa na kijamii ya nchi hiyo muhimu katika bara la Afrika. Katika sehemu nyingine tumejaribu pia kugusia hali ya dini tatu muhimu za Kiislamu, Kikatoliki na Kiothodoksi nchini humo. Sehemu ya mwisho ya makala hii inahusiana na hali ya hivi sasa ya Waislamu wa Ethiopia na pia uhusiano wa kiuchumi wa Iran na nchi hiyo.Maneno muhimu: Uhabeshi, Ethiopia, Uislamu, Ukristo, hajiri, jiografia, hali ya kihistoria na kisiasa, Italia, Haile Selassie, utawala wa kifalme na uhusiano wa kiuchumi. Uhabeshi inafahamika vyema kwa Waislamu kutokana na kuwa ndilo lililokuwa kimbilio la kwanza la maswahaba mashuhuri wa Mtume Mtukufu (SAW) mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu. Kabla ya Uislamu kuenea huko Bara Arabu kundi la kwanza kabisa la Waislamu lilihajiri na kuhamia Uhabeshi kutokana na mateso makubwa waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa makafiri wa eneo hilo. Uhabeshi ilisamehewa jihadi kutokana na kuwahifadhi Waislamu hao waliohamia huko. Najashi alikuwa mfalme wa kwanza Mkristo kusilimu na hadi leo Waislamu hulizuru kaburi lake kwa ajili ya kutoa heshima zao kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kuutetea Uislamu.Imeelezwa katika Siratu Ibn Is'haq (85-151 h) ya kwamba, Mtume Mtukufu (SAW) alipowaona maswahaba wake wakipata matatizo, shida na mabalaa makubwa, na Mtume kutokuwa na uwezo wa kuwazuia na kuwakinga na maudhi ya watu wao, na kutokuwepo katika kaumu zao watu ambao wangeweza kuwakinga na mateso hayo kama alivyofanyiwa yeye na ami yake Abu Twalib (baba yake Amiril-Muuminiin AS), aliwaamuru kuhajiri na kwenda Uhabeshi akiwaambia:"Hakika katika ardhi hiyo kuna mfalme ambaye hakuna mtu yeyote anayedhulumiwa kwenye nchi yake, ni ardhi ya ukweli. Basi kimbilieni huko na jikingeni na ngome yake mpaka Mwenyezi Mungu akuteremshieni faraja na kutunusuru sote."Kundi moja la maswahaba wake likahamia kwenye ardhi ya Uhabeshi ili kukwepa mateso na kwa ajili ya kulinda dini yao. Bwana Qutubddini Saidi bin Hibatulaah ar-Rawandiy (aliyefariki dunia mwaka 573 Hijiria) amesema: Pindi maudhi ya Makuraishi dhidi ya Mtume (SAW) na maswahaba wake ilipopindukia aliwaamuru watoke na kuelekea Uhabeshi, na akamuamuru Jaafar bin Abi Twalib awaongoze. Jaafar akatoka akiwa na wanaume sabini na kutumia vyombo vya baharini. Maquraishi walipofikiwa na habari za kugura kwao walimtuma Omar Binil-Aasi na Ammarah bin Waliid kwenda kwa Najashiy na kumtaka awarudishe kwao. Walimbebea zawadi Najashi. Amru akasema: Ewe Mfalme! Hakika watu fulani kati ya jamaa zetu wametupinga katika dini yetu na kukimbilia kwako, basi turudishie watu hao.Hapo Najashi akamtumia Jaafar ujumbe na kutaka aletwe kwake. Akasema: Ewe Jaafar! Watu hawa wananiomba nikurudisheni na kukukabidhini kwao. Akasema: Ewe mfalme! Waulize je, sisi ni watumwa wao? Amru akasema: Hapana bali ni watu walio huru na watukufu wenye heshima zao. Akasema waulize je, wana madeni wanayotudai ili tuwalipe madeni hayo? Akasema: Hapana hatuna madeni tunayowadai. Akasema: Je, kuna damu wazitakazo zilizoko mabegani kwetu? Amru akasema: hatuna damu zozote tuzitakazo zilizoko mabegani kwao na wala hatuwadai kitu chochote walichokiharibu. Akasema: Sasa ni nini wakitakacho kwetu? Amru akasema: Wametupinga katika dini yetu na kuzusha mfarakano katika jamaa zetu, basi turudishie watu hawa.Jaafar akasema: Ewe Mfalme! Tumepingana nao kutokana na Mtume aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwetu. Ametuamuru kujivua na miungu mingine isiyokuwa Mungu mmoja na kuacha kujitibu kwa kupiga bahati nasibu (korokoro). Ametuamuru kuswali, kutoa zaka na akaharamisha dhulma na ujeuri na kumwaga damu bila ya haki, kuzini, riba, damu na mzoga, na akatuamrisha kufanya uadilifu na kutenda wema na kuwapa watu wa karibu haki zao. Anakataza maovu na mambo machafu na uzinifu. Najashiy akasema: Kwa ajili ya haya Mwenyezi Mungu alimtuma Isa (AS) pia. Kisha akasema: Ewe Jaafar je, umehifadhi chochote kati ya baadhi ya aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwa mtume wako?Akasema: Ndio. Akasema: Soma. Jaafar akamsomea Suurat Maryam, na alipofika kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo: "Na jitikisie shina la mtende utakuangushia tende mbichi tamu" (19:25),Akasema: Huu ndio ukweli na haki ilivyo.Amru akasema: Ewe Mfalme! Hakika huyu ameacha dini yetu, mrudishe kwetu. Najashi akainua mkono wake na kumpiga usoni mwake, kisha akasema: Ukimtaja kwa ubaya nitakuua, Amru akatoka huku damu ikitiririka juu ya nguo yake. Amru akarudi kwa Makuraishi na kuwafahamisha habari za Mfalme Najashi, na Jaafar akabaki katika ardhi ya Uhabeshi akiwa katika hali tukufu kabisa na akiwa ni mwenye kukirimiwa. Aliendeleea kuwa huko hadi ilipomfika habari ya kuwa Mtume (SAW) amewekeana saini na Makuraishi makubaliano ya amani na suluhu. Hapo akarudi akiwa na watu wote waliokuwa naye na wakakutana na Mtume wa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa ameikomboa Khaibar. Jaafar alipata mtoto aitwae Abdallah bin Jaafar kutoka kwa Asmaa binti Umaisi alipokuwa Uhabeshi.Thiqatul-Islaam al-Kulainiy amepokea hadithi kutoka kwa Ali bin Ibraahim kwamba: Najashi alimwita Jaafar bin Abi Twalib na maswahaba wake na wao wakamjia akiwa nyumbani kwake na akiwa amekaa juu ya udongo huku akiwa amevalia nguo zilizoloa. Jaafar akasema: Tukamuogopa pindi tulipomuona akiwa katika hali ile, na wakati alipoona hali tuliyokuwa nayo akasema: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye amemnusuru Muhammad na kuyafurahisha macho yake. Je, nikupeni bishara? Nikasema: Ndio ewe Mfalme! Akasema: Amenijia mpelelezi mmojawapo kati ya wapelelezi wangu kutoka nchini kwenu.Amenipatia habari ya kuwa Mwenyezi Mungu amemnusuru Mtume wake Muhammad (SAW) na amemuangamiza adui wake na fulani na fulani na fulani wameshikwa mateka na walikutana katika bonde liitwalo: Badru-Kathiirul-Araak, na mimi kana kwamba ninamuangalia na kumuona kwani nilikuwa nikimchungia bwana wangu huko naye ni mtu mmoja katika kabila la Bani Dhamrah. Jaafar akamwambia: Ewe mfalme! Vipi nakuona ukiwa umekaa juu ya udongo na ukiwa na nguo hizi zilizoloa? Akamwambia: Ewe Jaafar! Hakika sisi tunaona kati ya mambo yaliyoteremshwa kwa Isa (AS), ya kwamba, ni haki ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake wamnyenyekee pindi anapowaletea neema. Na wakati Mwenyezi Mungu aliponipatia neema kwa kuja Muhammad (SAW) nikawa katika hali hii. Pindi jambo hilo lilipomfikia Mtume (SAW) akasema kuwaambia maswahaba wake: Hakika sadaka humzidishia mwenye kuitoa wingi basi toeni sadaka Mungu akurehemuni, na kwa hakika unyenyekevu humuongezea aliye nao daraja na utukufu, basi kuweni wanyenyekevu Mwenyezi Mungu atakuinulieni daraja zenu, na kwa hakika usamehevu humuongezea aliye nao utukufu na izza, basi kuweni wasemehevu Mwenyezi Mungu atakutukuzeni.Hadi ilifikia kwamba Mtume Mtukufu (SAW) alimtuma Amru bin Umayyah Adhwamriy - na alikuwa ndiye balozi wa kwanza aliyetumwa na Mtume (SAW) kwa wafalme akiwaita na kuwalingania kwenye Uislamu kwa Najashi aliyechukua barua ya Mtume (SAW) na kuiweka juu ya macho yake na kuteremka kutoka kitandani kwake kisha akakaa juu ya ardhi kwa unyenyekevu kisha akasilimu na kushuhudia shahada ya haki na akamuandikia barua Mtume (SAW) akiitika na kusadikisha ujumbe wake pamoja na kusilimu kwake mbele ya Jaafar bin Abi Twaalib nduguye Amiril-Muuminiin Ali (AS).Mtume wetu Mtukufu (SAW) alimuandikia Najashi barua na kuituma kupitia kwa Amru bin Umayyah kuhusu suala la Jaafar bin Abi Twalib na maswahaba wake kama ifuatavyo:'Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Kutoka kwa Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Najashi al-Adhkham kiongozi wa Uhabeshi amani iwe juu yako. Hakika mimi ninamsifu Mwenyezi Mungu kwako ambaye ni Mfalme, Mtakasifu, Muumini Mwenye kutawala mambo yote. Na ninashuhudia ya kwamba Isa bin Maryam ni roho ya Mwenyezi Mungu na ni neno lake aliloliweka kwa Maryamul-Batuul- aliyehifadhiwa na uchafu, aliye mwema na mwenye kuhifadhika na maasi, na kubeba mimba ya Isa, na kumuumba kutokana na roho yake na kumpulizia roho yake kama alivyomuumba Adam kwa mkono wake (uwezo wake) na kumpulizia ndani yake roho.Kwa hakika mimi ninakuita na kukulingania kwa Mwenyezi Mungu wa pekee asiye na mshirika, na kumtawalisha kwa kumtii, na kwamba unifuate mimi na uniamini na yale yaliyonijia, kwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nimetuma kwenu mtoto wa ami yangu Jafar bin Abi Twalib, akiwa na kundi la Waislaamu, wakikujia basi kiri na kusalimu amri kwake na acha kujigamba kwa ukubwa (kiburi). Kwa hakika mimi ninakuita wewe na watu wako kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa hakika nimefikisha na kunasihi, basi kubalini nasaha zangu na amani iwe juu ya mwenye kufuata uongofu.'Najashi akamuandikia: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Barua kuelekea kwa Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kutoka kwa Najashi Adhkham bin Abhar. Amani iwe juu yako ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu kutoka kwake na rehama za Allah na baraka zake! Hapana Mola wa haki isipokuwa Yeye ambaye ameniongoza kwenye Uislamu. Kwa hakika nimefikiwa na barua yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kuhusiana na uliyoyataja kuhusu suala la Isa, ninaapa kwa Mola wa mbingu na ardhi hakika Isa hazidi na kuyapituka uliyoyataja, na kwa hakika tumefahamu uliyotumwa nayo kwetu.Tumemkirimu na kumpokea kama mgeni wetu mtoto wa ami yako na maswahaba wake, na ninashuhudia ya kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa ukweli na mwenye kusadikisha, na kwa hakika nimekupa baia (kiapo cha utiifu) na nimempa baia mtoto wa ami yako. Nimesilimu mbele yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote, na nimemtuma kwako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ariiha bin Adhkham bin Abhar. Hakika mimi sina ninachokimiliki isipokuwa nafsi yangu, ukitaka nije kwako nitafanya hivyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwa hakika mimi ninashuhudia ya kuwa uyasemayo ni haki na kweli."Bwana Zurarah amepokea hadithi kutoka kwa Abi Jaafar al-Baaqir (AS) ya kwamba amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa amemtuma kabla ya kwenda Khaibar, Amru bin Umayyah Adhwamriy kwa Najashi, Mfalme wa Uhabeshi, na kumlingania kwenye dini ya Kiislamu, naye akasilimu, na alikuwa amemuamuru Amru atangulie pamoja na Jaafar na sahaba zake, na Najashi akamuandalia Jaafar na sahaba zake maandalizi mazuri na akaamuru waletewe mavazi (nguo) na akawabeba kwenye majahazi mawili.Pia imepokelewa ya kwamba Mtume (SAW) alipojiwa na Jibril alimfahamisha msiba wa Najashi, akalia sana na kumhuzunikia na akasema: Hakika ndugu yenu As'ham (Nalo ni jina la Najashi) amefariki dinia. Kisha akatoka hadi mahala paitwapo Jabanah na kumsalia, akapiga takbira mara saba na Mwenyezi Mungu akamshushia kila kilichokuwa kirefu hadi akaliona jeneza lake hali ya kuwa yuko Uhabeshi.Shekh Jaafar Kaashiful-Ghitwaa (aliyefariki dunia mwaka 1228 Hijiria) anasema kwamba haisihi (yaani kumsalia maiti) aliyeghaibu, na kwamba tukio la kumsalia Najashi hali ya kuwa yuko ghaibu ni suala lihusikalo na tukio hilo tu, au kwa twayyir-ardhi, au kuhudhuria kama vile upepesuaji wa jicho la Balqisi - bila ya kuona - na hayo yote mawili hayako mbali na uwezo wa Mwenyezi Mungu.Na kutokana na kisa cha Najashi tunafaidika na kupata natija ya kwamba, sehemu ya kwanza kuenea Uislamu nje ya Bara Arabu, ni katika nchi za Afrika, na hiyo ni kutokana na ubora wa kusilimu kwa Najashi na watu wake. Wakati huohuo mjumbe wa kwanza kutumwa kwa wafalme ni yule aliyetumwa kwa Najashi ambaye alimpokea kwa wema. Hili linatujulisha usafi wa watu watukufu wa bara la Afrika ambao ni wakarimu, wateule na wenye maumbile safi.Kama ambavyo tunafaidika kutokana na kisa cha Najashi pia ya kwamba, Afrika ilikuwa ni sehemu na ardhi nzuri na bora ulimwenguni kwa upande wa uhuru wa kujieleza na ukimbizi wa kisiasa na kiitikadi kwa ajili ya Waislaamu katika zama zile. Hata kama Waislamu walifanikiwa kuunda majimbo yaliyokuwa yakijitawala katika eneo la Falat katika karne za 15 na 17 lakini hawakufanikiwa kuunda muungano madhubuti wa kiutawala kutokana na tofauti zao za kikabila. Kutokana na jambo hilo walilazimika kulipa jizia kubwa kwa serikali kuu ya Uhabeshi ili kuepuka mashambulio yaliyokuwa yakifanywa katik zama hizo dhidi yao na serikali ya Kikristo (Dehkhoda juz.19 uk.211). Kutokana na utajiri wake mkubwa wa kihistoria na hasa wa Kiislamu, ni muhimu kuchambua masuala kadhaa yanayohusiana na nchi hii muhimu na kongwe ya Pembe ya Afrika.Uhabeshi au kwa jina jingine Ethiopia ni muhimu kutokana na matukio na uvumbuzi wake wa masuala yanayohusiana na kipindi cha kabla ya historia, matukio muhimu ya kidini kama vile kisa cha Ukhdud ambacho kimetajwa katika Sura ya Buruj katika Qur'ani Takatifu na mauaji yaliyotekelezwa dhidi ya Wakristo na Mfalme Dhunawas wa Kiyahudi. Kufuatia mauaji hayo, Abraha, mfalme Mkristo wa Ethiopia aliamuru mmoja wa makamanda wake wa kijeshi afanye shambulio dhidi ya mfalme huyo wa Kiyahudu katika Bara Arabu. Kisa cha Abraha aliyetaka kuivamia nyumba takatifu ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba kimetajwa katika Surat al-Fil katika kitabu kitakatifu cha Qur'an. Lakini kisa muhimu zaidi kinachozingatiwa na Waislamu ni kile tulichokitaka hapo mwanzoni kinachohusiana na kuhajiri kwa Waislamu wa mwanzo kuelekea Uhabeshi ambapo walipokelewa kwa moyo mkunjufu na Mfalme Najashi ambaye hatimaye alikubali Uislmu na akaaga dunia akiwa ni Muislamu. Nchi hii ya Uhabesha au Habasha pia ndiko alikotokea Bilal al Habasha ambaye ni mashuhuri sana katika historia ya Kiislamu kwa kuwa alikuwa ni swahaba na muadhini mahususi wa Mtume (SAW). Huyu alikuwa ni mtumwa wa kawaida lakini ambaye baada ya kuona ukweli wa Uislamu, aliukubali bila kusita. Hata baada ya kupata mateso mengi na makali kutoka kwa makafiri wa Kikureishi kwa ajili ya kumlazimisha awachane na Uislamu na kuendelea kuabudu masanamu, Bilal alipinga vikali jambo jambo hilo na kuukumbatia Uislamu kwa moyo na nguvu zake zote, jambo lililomfanya ateswe zaidi na bwana wake.Asili ya jina Ethiopia Pamoja na kuwa asili ya jina Ethiopia haifahamiki vyema lakini waliowengi wanaamini kwamba inatokana na jina la Kigiriki cha kale ???????? Aithiopia lililotokana na ??????. "Aithiops" ; maana yake ni "uso" (??) au "kuwaka" (???w). Kwa hivyo labda "uso uliochomwa" au "sura nyeusi." Lakini jina hili halikumaanisha hasa nchi ya Ethiopia ya leo lakini nchi zote penye watu wenye rangi nyeusi. Kwa muda mrefu watu wa Ulaya waliita Afrika yote kwa jina "Ethiopia". Pia si wazi kama neno la Kiafrika lenye maana tofauti limechukuliwa na Wagiriki kwa maana ya neno lao la 'Aithiops.' Ni nchi ambayo ina historia ya pekee katika bara la Afrika na hata duniani kwa ujumla. Ethiopia ni nchi pekee ya Afrika ambayo haikutawaliwa na wakoloni wala kutwaliwa wakati wa Mng'ang'anio wa Afrika. Katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia Ethiopia ilivamiwa na Waitalia.Nchi yenyewe ilijulikana kwa muda mrefu wa historia yake kwa jina la "Habasha". Habasha likiwa ni jina la Kiarabu, inajulikana katika Kiswahili kama "Uhabeshi" au "Abesinia" katika lugha za Ulaya. Asili ya jina hili pia haiko wazi; wengine husema ya kwamba ni Kiarabu lenya maana ya "chotara" ilihali wengine husema ni katika lugha ya kale ya nchi yenyewe yenye maana ya "nchi kwenye nyanda za juu." Wengine wanadai ya kwamba jina hilo limetoka Uarabuni Kusini lilipokuwa jina la kabila moja lililohama na watu walioleta lugha za Kisemiti Ethiopia.Kumbukumbu ya Ethiopia kwa lugha ya kale ya Ge'ez inasema kuwa jina hilo linatokana na mtoto wa Ham kwa jina la "'Ityopp'is" asiyetajwa katika Biblia. Kumbukumbu hiyo inadai kuwa yeye ndiye aliyejenga mji wa Aksum. Lakini habari hii si ya kihistoria ila tu ni jaribio mojawapo la kuunganisha wafalme wa Aksum na historia ya Biblia. Neno Abyssinia lenyewe lilitokana na neno Habahasha. Kuna baadhi ya watu wanasosema kwamba watu wa Habasha walitokana na vizazi vya wahajiri wa Kiarabu na Waafrika katika eno la Pembe ya Afrika katika milenea ya kwanza B.C. Katika karne ya 16 katika kipindi ambacho Wareno na Waothmania walipokuwa wakipigana kuwania udhibiti wa Bahari Arabu, Nyekundu na Hindi kwa ajili ya masuala ya kibiashara na kiuchumi, Wareno walishirikiana na Wahabeshi dhidi ya Waothmania.Historia ya kale Mabaki ya visukuku vya vizazi vya mwanzo vya mwanadamu yaliyogunduliwa nchini Ethiopia yanasemekana kuwa ni ya umri wa miaka milioni 5.9 iliyopita. Nchi hii na Eritrea na vilevile eneo la kusinimashariki mwa bahari Nyekundu yanachukuliwa kuwa eneo lililojulikana zamani na Wamisri kwa jina la Punt kwa maana ya nchi ya miungu. Jina hili lilitajwa kwa mara ya kwanzaka tika karne ya 25 BC.Karibu na karne ya nane BC, ufalme ulibuniwa kaskazini mwa Ethiopioa na Eritrea mji mkuu wake ukiwa Yeha. Katika kipindi cha utawala wa Mfalme Yeshaq, Ethiopia ilianzisha uhusiano wake wa kwanza wa kidiplomasia na nchi za nje za Ulaya tokea kipindi cha utawala wa Waaksum. Mfalme huyo aliwatuma wajumbe wake wawili kwa Alfons wa VII wa Arogan ambaye naye alituma nchini Ethiopia wajumbe wake ambao kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kukamilisha safari yao nchini humo. Uhusioa wa kwanza wa kidiplomasia wa kudumu kati ya Ethiopia na nchi za Ulaya ulianza kushuhudiwa katika mwaka wa 1508 kupitia uhusiano wa Mfalme Lebna Dengel wa Ethiopia na nchi ya Ureno.Kuepuka kugombaniwa Afrika Miaka ya 1880 ilishuhudia mg'ang'anio wa bara la Afrika kutoka kwa nchi koloni za Magharibi. Kinyume na zilivyokuwa nchi nyingi za bara la Afrika katika kipindi hicho, Ethiopia ilishuhudia maendeleo makubwa, mbali kabisa na madhara ya siasa za wakoloni, ambapo nchi hiyo ilikuwa uwanja wa ushawishi wa Italia na Uingereza kwa ajili ya kuyadhibiti maeneo ya karibu na nchi hiyo. Bandari ya Asseb karibu na lango la kusini mwa Bahari Nyekundu ilinunuliwa mwezi Mei 1870 na kampuni moja ya Kiitaliano kutoka kwa mfalme wa Afar na kupewa mfalme wa Ethiopia. Jambo hilo lilipelekea kukoloniwa nchi jirani ya Eritrea na Italia mwaka 1890. Mivutano kati ya nchi mbili hizo ilipelekea kuzuka mapigano ya Adowa mwaka 1896, ambapo Waethiopia waliushangaza ulimwengu kwa kuwashinda wakoloni katika medani ya vita, na hivyo kuendelea kubakia huru, kwa uongozi wa Mfalme Menelik II.Ethiopia na Italia hatimaye ziliwekeana saini makubaliano ya amani tarehe 26 Oktoba 1896. Miaka ya mwanzoni mwa karne ya ishirini ilishuhudia utawala wa Mfalme Haile Selassie I ambaye aliiongoza Ethioa katika kufikia maendeleo makubwa, maendeleo ambayo yalisitishwa kwa kipindi kifupi kutokana na uvamizi wa Italia. Uvamizi huo baadaye ulimalizwa kwa ushirikiano wa kijeshi wa Uingereza na askari wazalendo wa Ethiopia ambao walifanikiwa kuiondoa nchi hiyo katika makucha ya Wataliano katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1941. Ethiopia hatimaye ilitangazwa na Waingereza kuwa nchi huru kamili tarehe 31 Januari 1941 kwa kutopewa fursa zozote kutoka kwa serikali ya Uingereza kupitia mkataba uliotiwa saini na pande hizo mwezi Disemba.Miaka ya Selassie Haile Selassie aliingia madarakani baada ya kumalizika kwa kipindi cha Menelik. Hata kama mwanzoni Selassie alichukuliwa na Waethiopia waliowengi kuwa shujaa wa kitaifa aliyejali maslahi ya wananchi wa nchi hiyo, lakini hatimaye walimgeuka na kuanza kumlaani na kumkosoa vikali baada ya utawala wake kuanza kuwapuuza na kuwajali zaidi watawala wa nchi hiyo na kuacha mamilioni ya Waethiopia wakiteseka na kufa kwa njaa. Mwaka 1974, wanafunzi, wafanyakazi, wakulima na jeshi zima walisimama dhidi yake. Utawala wa Haile Selassie ulifikia kikomo mwaka huohuo wa 1974, kutokana na machungu pamoja na matatizo ya kiuchumi, kufuatia mapinduzi yaliyofanywa dhidi yake na wanajeshi waliokuwa na mueleko wa Kimaksi na Kilenini wakiongozwa na Mengistu Haile Mariam. Baada ya kufanikiwa mapinduzi hayo ya kijeshi, wafanyamapinduzi hao waliokuwa wakiunga mkono siasa za Shirikiso la Urusi ya zamani walianzisha utawala wa chama kimoja kilichokuwa kikifuata siasa za ukomunisti. Haile Selassie alikamatwa na kufungwa jela na wanajeshi hao ambao inasemekana kuwa walimtesa hadi kufa. Wanajeshi hao walimtaka awape pesa walizodai kuwa zilikuwa dola milioni 25 ambazo walisema alikuwa amezificha katika benki za Uswisi.Ukomunisti Tawala zilizofuata zilikabiliwa na mapambano, majanga makubwa ya njaa na ukame, wimbi la wakimbizi na pia mapinduzi kadhaa kama hayo. Mwaka 1977 Somalia iliihujumu Ethiopia na hivyo kuzusha vita vya Ogaden. Lakini pamoja na hayo vita hivyo vilimalizika haraka mwaka uliofuata kwa ushindi wa Ethiopia baada ya nchi hiyo kupata msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Urusi, Cuba, Ujerumani Mashariki na Yemen. Katika kipindi hicho, Mengistu alikuwa akiishi uhamishoni nchini Zimbabwe, ambapo juhudi za wanajeshi waliokuwa wakitawala zilishindwa kumrejesha nchini ili kushtakiwa kuhusiana na makosa aliyofanya katika kipindi cha utawala wake. Viongozi 106 wa serikali yake walishtakiwa kutumia vibaya uongozi wao katika kipindi cha utawala wa Haile Selassie lakini ni 36 tu miongoni mwao ndio waliofikishwa mahakamani kujibumashtaka yaliyokuwa yakiwakabili kuhusiana na jambo hilo. Watuhumiwa wengine walihukumiwa bila ya kufika mahakamani. Kesi dhidi yao ilianzishwa mwaka 1994 na kumalizika 2006. Haile Mariam ambaye alikuwa miongoni mwa watuhumiwa waliohukumiwa bila ya kuwepo mahakamani alihukumiwa kwa makosa ya mauaji ya halaiki katika kipindi cha utawala wake nchini Ethiopia kati ya mwaka 1974 na 1991, kipindi ambacho kiliitwa kuwa cha 'ugaidi mwekundu.' Hakuna mapatano yoyote ya kubadilishana wahalifu yaliyokuwepo kati ya nchi mbili za Ethiopia na Zimbabwe.Ugaidi Mwekundu Juhudi zilizofanywa na chama cha Ethiopian People's Revolutionary Party EPRP za kuamsha hisia za wananchi dhidi ya kundi la kijeshi la Derg na washirika wake ndizo zilizozusha ghasia za mwaka 1976. Majengo ya serikali yaliharibiwa na viongozi wengi wa serikali kuuawa katika ghasia hizo. Kundi la Derg ambalo lilikabiliana na ghasia hizo kupitia kampeni zake za Ugaidi Mwekundu zilizitaja mbinu za chama cha EPRP kuwa Ugaidi Mweupe. Mengistu alisema kwamba wanamapinduzi wote walikuwa huru kukabiliana na maadui wa mapinduzi. Chuki na hasira yake ilielekezwa kwa chama cha EPRP. Wakulima, wafanyakazi na watumishi wa umma wote na hata wanafunzi waliodhaniwa kuwa waaminifu kwa utawala wa Mengistu walipewa silaha ili kupambana na maadui hao.Hatua hiyo ya Mengistu ilikuwa hatari mno kwa sababu ilipelekea Waethiopia kuuana wenyewe kwa wenyewe na hivyo kueneza nchini wimbi la ghasia. Kinyume na alivyotarajia, wengi wa watu waliopewa silaha walikuwa ni waaminifu kwa chama cha EPRP. Tokea mwaka 1977 hadi mwishoni mwa 1978 zaidi ya watu 5000 walikuwa tayari wamepoteza maisha yao. Kundi la Derg lilianza kutengwa na Waethiopia na hata wale waliokuwa wakiliunga mkono kundi hilo mwanzoni. Kuongezeka kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Ethiopia kulizipelekea nchi za Magharibi na hasa Marekani kulaani vikali vitendo hivyo na kutaka visimamishwe mara moja.Pamoja na hayo, lakini utawala wa Mengistu uliendelea kuwakandamiza Waethiopia ambao uliwachukulia kuwa maadui wake ili kulinda nafasi yake nchini humo. Baadhi ya wataalamu wanasema kwamba kati ya mwaka 1975 hadi 78 watu laki moja na nusu wakiwemo wanafunzi, wasomi na wanasiasa waliuawa katika ukandamizaji huo wa utawala wa Kimaksi wa Mengistu.Waethiopia na makundi mengi ya haki za binadamu yanadai kwamba ukandamizaji huo hata ulimpelekea Mengistu kuwazingira na kuwaua kwa njaa mamilioni ya Waethiopia kaskazini mwa nchi hiyo, njaa ambayo ilipelekea kuchukuliwa kwa juhudi kubwa za kimataifa ziitwazo 'Live Aid' kwa ajili ya kuwaokoa wananchi hao. Kuhusiana na mauaji hayo, Mengistu anadaiwa kuwa mtenda jinai wa mauji ya 7 makubwa zaidi ulimwenguni katika historia ya mwanadamu. Waethiopia milioni moja na nusu wanadaiwa kuwa wahanga wa mauaji hayo ya kundi la Derg. Mbali na mapambano ya msituni yaliyoanzishwa na chama cha EPRP harakati nyingine kama vile za EPLF, OLF, TPLF/EPRDF na WSLF zilizidisha mapambano yao ya kijeshi kwa ajili ya kuing'oa madarakani serikali ya Mengistu Haile Mariam.Mwaka 1993 kura ya uchunguzi wa maoni ilifanyika ndani na nje ya Eritrea kwa usimamizi wa ujumbe wa Umoja wa Matifa UNOVBER ili kuona iwapo Waeritrea walitaka kupewa uhuru au kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa Ethiopia. Zaidi ya asilimia 99 ya Waeritrea walipigia kura uhuru wao ambao ulitangazwa rasmi tarehe 24 Mei 1993. Mwaka 1994 katiba mpya ilipitishwa nchini Ethiopia, ambayo iliruhusu Ethiopia kutawaliwa na mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwaka uliofuata. Mwaka 1998 mzozo wa mpaka ulipelekea nchi mbili hizo kupigana mapigano ambayo yalimalizika Juni 2000. Vita hivyo viliisababishia Ethiopia hasara kubwa ya kiuchumi lakini viliimarisha serikali ya mseto ya nchi hiyo. Mwezi Mei 2005 Ethiopia alifanya uchaguzi mwingine wa vyama vingi ambao ulizusha mamalamiko mengi miongoni mwa mrengo wa upinzani ambao ulidai kwamba udanganyifu na wizi wa kura ulifanywa na serikali. Katika hali ambayo Kituo cha Usimamizi cha Carter cha Marekani kilisema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, lakini Jumuiya ya Ulaya iliituhumu serikali kuwa ilifanya udanganyifu katika uchaguzi huo. Kwa vyovyote vile upinzani ilipata viti vya bunge 200 vikilinganishwa na 12 tu ulivyopata katika uchaguzi wa 2000. Mbali na wapinzani wengi kujiunga na bunge la Ethiopia lakini viongozi wengi wa upinzani ambao Shirika la Msahamaha Duniani, Amnesty International, linawaita kuwa 'wafungwa wa dhamira,' wangali wanashikiliwa katika jela za nchi hiyo.Siasa za Ethiopia Nchini Ethiopia Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa serikali na ana mamlaka makubwa ya kiutendaji. Uwezo wa kubuni sheria zinazoihusu nchi nzima umepewa serikali na mabunge mawili ya nchi hiyo. Vyombo vya mahakama vina uwezo mdogo na kimsingi hutegemea serikali na mabunge yaliyotajwa. Bunge lenye viti 547 lilichaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1994 ambapo lilipasisha katiba ya Shirikisho la Kidemokrasia la Ethiopia katika mwaka huohuo. Katika uchaguzi wa bunge kuu na mabunge ya kieneo uliofanyika mwaka uliofuata wa 1995, vyama vingi viliususia uchaguzi huo.Kufuatia ususiaji huo, chama cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front EPRDF kilijipatia ushindi mkubwa. Mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali yalihalalisha uchaguzi huo kwa kusema kwamba vyama vya upinzani vingeweza kushiriki na kujipatia nafasi nzuri kama vingeamua kushiriki katika uchaguzi huo. Rais wa kwanza wa Ethiopia alikuwa ni Bwana Negasso Gidada. Serikali ya EPRDF inayoongozwa na Waziri Mkuu Meles Zenawi imekuwa ikiimarisha sera ya mashirikisho ya kikabila ambapo ameyapa madaraka makubwa ya kiutawala. Katika hali ya hivi sasa, Ethiopia ina maeneo kama hayo tisa ambayo yana uwezo wa kukusanya na kutumia kodi yanazozikusanya. Katika mazingira ya hivi sasa, Ethiopia ina kiwango kidogo cha uhuru wa vyombo vya habari. Televisheni inamilikiwa na serikali.Jiografia ya Ethiopia Kirasmi, Ethiopia ni nchi iliyoko katika eneo la Pembe ya Afrika na isiyokuwa na njia ya bahari tokea kutangazwa rasmi kwa uhuru wa jirani wake wa kaskazini, Eritrea mwaka 1993. Ikiwa na ukubwa wa kilomita-mraba 1,127,127, Ethiopia ni nchi ya 27 kwa ukubwa ulimwenguni baada ya Colombia. Ukubwa wake ni karibu thuluthi mbili ya ukubwa wa jimbo la Alaska nchini Marekani. Ethiopia inapakana na Sudan katika upande wa Magharibi na Eritrea katika upande wa Kaskazini. Somalia iko upande wa Mashariki na Kenya upande wa Kusini. Ethiopia ni nchi yenye nyika, milima na nyanda za juu nyingi zinazogawanywa na Bonde la Ufa. Muundo huo wa milima na mabonde pamoja na nyika ndio unaoainisha tafauti kubwa ya mazingira, hali ya hewa na mchanga katika maeneo mbalimbali ya Ethiopia.Hali ya hewa, ikolojia na muundo-ardhi Mvua za kawaida hunyesha tokea katikati ya mwezi Juni hadi katikati ya mwezi Septemba na hata zaidi ya hapo katika maeneo ya Kusini. Vipindi tofauti vya mvua nyepesi huanza katika mwezi wa Februari au Machi. Kipindi kilichosalia cha mwaka huwa ni kikavu kwa ujumla. Ethiopia kama tulivyosema mwanzoni ni nchi yenye hali mbalimbali na tofauti ya hewa. Hali yake ya ikolojia pia ni tofauti, tokea majangwa katika mpaka wake wa Mashariki hadi misitu ya tropiki katika upande wa Kusini. Ziwa Tana katika upande wa Kaskazini ndicho chanzo cha Mto Blue Nile. Hali yake maalumu ya ikolojia na hali ya hewa imeipa nchi hiyo muundo maalumu wa mazingira tofauti tofauti. Hata hivyo suala la mmomonyoko wa udongo ni tatizo kubwa nchini Ethiopia linalohatarisha mazingira ya nchi hiyo. Mwanzoni mwa karne ya 20 karibu asilimia 35 ya ardhi yote ya Ethiopia ilikuwa na miti, lakini hivi sasa kiwango hicho kimepungua na kufikia asilimia 11.9 tu. Inakadiriwa kwamba kila mwaka Ethiopia hupoteza utajiri wake wa misitu kwa ukubwa wa kilomita-mraba 1,410. Pamoja na hayo, serikali ya Addis Ababa imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika miaka ya hivi karibuni kwa lengo la kulinda misitu yake na pia kushajiisha juhudi za upandaji miti mipya. Mashirika kama vile SOS na Farm Afrika yanashirikiana bega kwa began a serikali katika kusimamia misitu.Majimbo ya Ethiopia Kabla ya mwaka 1996 Ethiopia ilikuwa imegawanyika katika mikoa 13 ya utawala, mingi ikiwa na uhusiano wa kihistoria. Lakini katika hali ya hivi sasa nchi hiyo imegawanywa katika majimbo tisa ya kiutawala ambayo kimsingi ni ya kikabila. Mabunge ya majimbo hayo pia yana uwezo wa kujitungia sheria ya kujitawala. Kipengee cha 39 cha katiba ya Shirikisho la Kidemokrasi la Ethiopia kinayapa majimbo hayo uwezo wa kujitenga. Majimbo hayo pamoja na miji miwili sajiliwa ni kama ifuatavyo: Addis Ababa, Afar, Amhara, Benishangul-Gumuz, Dire Dawa, Gambela Harari, Oromia, Somali, Southern Nations, Nationalities, na Tigray.Uchumi Baada ya mapinduzi ya mwaka 1974 uchumi wa Ethiopia iliendeshwa kwa udhibiti mkubwa wa serikali kuu. Wakati huohuo kutokana na kuwa serikali ya Mengistu Haile Mariam ilikuwa na uhusiano mmbaya na nchi za Magharibi, serikali hiyo ilificha janga kubwa la njaa lililotokea katika maeneo ya Tigray na Wallo na kupelekea watu zaidi ya laki mbili na nusu kupoteza maisha yao katika miaka ya 1972 na 1973. Baada ya janga hilo, marekebisho mengi ya kiuchumi yalifanyika nchini Ethiopia. Tokea katikati ya mwaka 1991 na kuendelea uchumi wa Ethhiopia taratibu uliondolewa katika udhibiti mkubwa wa serikali kuu na kuruhusiwa kuelekea katika mkondo wa sekta binafsi na soko huria. Hatua hiyo ilichukuliwa kwa lengo la kurekebisho uchumi wa nchi hiyo uliokuwa umedorora sana katika kipindi cha muongo mmoja. Mwaka 1993 sekta ya viwanda, biashara, benki na kilimo taratibu ilianza kubinafsishwa. Pamoja na hali hiyo lakini hadi sasa bado kuna matatizo katika mwenendo wa ubinafsishwaji wa sekta mbalimbali za uchumi wa Ethiopia.Vituo na mashirika mengi ya serikali yamepewa makundi yanayounga mkono serikali ya Addis Ababa kwa kisingizio cha ubinafsishwaji. Mbali na hayo, katiba inabainisha uwezo wa kumiliki mashamba kuwa ni wa serikali na umma tu, na kwamba watu wa kawaida wana uwezo wa kukodi mashamba hayo kwa kipindi cha miaka 99 tu bila ya kuwa na uwezo wa kuyauza, kununua wala kuyamiliki.Baadhi ya vyama vya kisiasa vinataka ubinafsishwaji kamili ufanyika katika uwanja huo ilihali vingine vinapinga jambo hilo na kutaka mashamba hayo yamilikiwe na makundi ya kijamii. Kilimo kinachangia karibu asilimia 41 ya pato jumla la taifa (GDP) la Ethiopia, asilimia 80 ya bidhaa zote zinazouzwa nje na asilimia 80 ya ajira nchini humo. Mazao muhimu nchini ni kahawa, nafaka, viazi, miwa na mboga. Kahawa ndiyo inayoiletea Ethiopia fedha nyingi zaidi za kigeni. Kiwango cha mifugo ya Ethiopia kinahesabiwa kuwa kikubwa zaidi katika bara zima la Afrika. Mwaka 1987, pato la mifugo hiyo liliunda asimia 15 ya pato jumla la taifa.Pamoja na marekebisho yote ya uchumi ambayo yamefanyika nchini Ethiopia lakini nchi hiyo ingali inakabiliwa na mlipuko mkubwa wa ukuaji wa kasi wa jamii na hivyo kuifanya kuwa mojawapo ya nchi masikini zaidi ulimwenguni. Maharagwe na maua pia ni sehemu muhimu ya kilimo cha Ethiopia. Inakadiriwa kuwa katika miaka ijayo nchi hiyo itakuwa miongoni mwa nchi muhimu zinazozalisha maua ulimwenguni. Kutokana na kuwa na vyazo vingi vya maji, watu mara nyingine huvitaja vvyanzo hivyo kuwa ni 'mafuta meupe' ya Ethiopia na kahawa yake kuwa 'dhahabu nyeusi'. Ethiopia pia ina migodi kadhaa ya madini na kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana mafuta katika baadhi ya maeneo ya makazi.Lugha Ethiopia ina lugha zipatazo 84 za asili ambazo baadhi ni kama ifuatavyo: Afar Amharic, Anfillo, Berto, Bussa, Kambata, Hadiya, Harari,Konso,Ongota, Oromo, Saho, Soddo, Silt'e, Somali, Tigrinya, Sidama, Wolaita, Gurage, Gamo na Goffa. Kiingereza ni lugha ya kigeni inayozungumzwa kwa wingi zaidi nchini Ethiopia na ndiyo inayotumika katika kufundishia masomo katika shule za sekondari. Kiamharic kilikuwa kikitumika sana katika ufundishaji katika shule za msingi lakini sasa nafasi ya lugha hiyo imechukuliwa na lugha za kieneo kama vile Kioromifa na Kitigrinya. Ethiopia ina herufi za alfabeti na kalenda yake yenyewe inayotofautiana na nchi nyingine. Kwa karne nyingi, sekta ya elimu ya Ethiopia ilitawaliwa na kanisa la Orthodox hadi baada ya kuja kwa mfumo wa kisekula katika miaka ya 1900. Mfumo jumla wa elimu nchini Ethiopia ni wa miaka sita ya elimu ya msingi, minne katika sekondari ya chini na miwili ya sekondari ya juu.Michezo Ethiopia ina moja ya wakimbiaji bora zaidi ulimwenguni na hasa katika mbio za masafa ya wastani na masafa marefu. Kenya na Morocco ni wapinzani wakali wa Ethiopia katika uwanja huo. Baadhi ya wakimbiaji mashuhuri wa Ethiopia ambao wamekuwa wakitawala katika uwanja huo wa mbio ni pamoja na Haile Gebreselassie ambaye amevunja zaidi ya rekodi 20 katika mbio za masafa marefu na Kenenisa Bekele. Wakimbiaji wengine mashuhuri wa Ethiopia ni pamoja na Derartu Tulu, Abebe Bikila, Mamo Wolde na Miruts Yifter. Derartu Tulu alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka bara la Afrika kushinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika huko Barcelona nchini Uhispania. Adebe Bikila alivunja rekodi katika mbio za nyika zilizofanyika katika miaka ya 1960 na 1964. Hadi leo angali anajulikana sana kutokana na kuvunja rekodi ya mbio hizo za Olimpiki zilizofanyika mjini Rome Italia akiwa miguu mitupu bila ya viatu.Watu na utamaduni Ethiopia kama zilivyo nchi nyingi za bara la Afrika, ina utajiri mkubwa wa lugha na tamaduni mbalimbali. Pamoja na kuwa tamaduni nyingi za nchi hiyo zimedhoofika na hatimaye kutoweka kutokana na ndoa na wageni, lakini bado kuna tamaduni nyingi za kale na za kuvitia katika nchi hiyo muhimu ya bara la Afrika. Kuna makundi makuu manne ya lugha nyingi za Ethiopia ambayo ni ya Kesemiti, Kikushi, Kiomotiki na Kinilo-Saharan. Kuna lahaja zaidi ya 200 za lugha hizo. Kisemiti kinanasibishwa kwa lugha za Kihibrania na Kiarabu. Lugha kuu ya kundi hili la lugha za Kisemiti ni Kiamharic ambacho kinazungumzwa katika maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Ethiopia na pia ndiyo lugha rasmi ya taifa.Lugha nyingine muhimu ni pamoja na Kitigrigna, Kiguraginya, Kiadarinya, Kiafan Kioromo, Kisomalinya, Kisidaminya, Kiafarinya, Kigumuz, Kiberta na Kianuak. Watigrigna na Waamharic wanaishi katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa nchi na kimsingi ni wakulima wanaotumia ng'ombe katika kilimo chao. Hukuza mtama, mahindi na ngano. Waoromo ambao zamani walikuwa wafugaji wakubwa wa mifugo hivi sasa wanajishughulisha na kilimo katika maeneo makavu ya nchi. Wasomali wa Ethiopia pia wanaishi katika maneo yenye ukavu huku wakijishughulisha na ufugaji mifugo wa kuhamahama. Waafar ni wakulima, wafugaji na pia wavuvi. Waethiopia kwa ujumla huvaa mavazi yanayotofautiana kutoka eneo hadi eneo jingine. Pamoja na hayo, vazi la taifa ambalo hushonwa kutokana na kitambaa cheupe cha pamba kilichozungukwa na mistari ya rangi tofauti pembeni kimsingi huonekana lemevaliwa katika siku za sherehe za kitaifa. Waethiopia hujivunia sana mitindo mbalimbali ya mavazi yao ya kimila na kijadi.Kanisa la Orthodox Kanisa la Orthodox ndilo kanisa kongwe zaidi kati ya makanisa ya Mashariki kuwahi kuingia nchini Ethiopia. Mwanzoni, mkuu wa kanisa hilo alikuwa ikiteuliwa mjini Alexandria Misri, lakini utaratibu huo ulibadilishwa na Mfalme Haile Selassie. Kanisa hilo lilikuwa na satua kubwa nchini Ethiopia katika miaka ya huko nyumba, na wakati mmoja likiwa la pekee lililoruhusiwa kumiliki ardhi nchini humo, wakati watu wengine wote wakinyimwa haki hiyo. Lilikuwa na ushawi mkubwa katika kila maamuzi muhimu yaliyochukuliwa nchini. Kufuatia kubadilika kwa serikali na tawala za Ethiopia, ushawishi wa kanisa hilo umepungua kwa kiasi kikubwa. Hii ni kinyume na ilivyotarajiwa na wengi kwa kutilia maanani kwamba kimsingi kanisa la Orthodox huwa halijishugulishi sana na masuala ya kisiasa, kinyume na makanisa ya Magharibi ambayo huenda hata yakadaiwa kwamba ndiyo yaliyowafunza Wamagharibi siasa. Pamoja na hayo lakini kanisa hilo limekuwa likiishi kwa amani na dini nyinginezo bila ya kushuhudia vita kama vile vilivyoanzishwa na Ukristo wa nchi za Magharibi.Kanisa Katoliki Inasemekana kwamba Kanisa Katoliki lilianza kupenya na kuingia nchini Ethiopia katika kipindi cha safari za uvumbuzi za Wareno barani Afrika mwishoni mwa karne ya 15. Katika kipindi hicho uhusiano wa makao makuu ya Kanisa Katoliki mjini Roma na kanisa la Ethiopia ulianza kustawi. Kuhusiana na suala hilo, Ukatoliki ulipata nguvu na kuimarika zaidi nchini Ethiopia kutokana na udhibiti wa watala wa Italia nchini Eritrea. Watawala hao ambao kimsingi walikuwa ni Wakatoliki waliweza kuimarisha na kueneza madhehebu hiyo ya Kikristo nchini Ethiopia kupitia uhusiano wa kisiasa na kijamii na nchi hiyo. Katika hali ya hivi sasa, Wakatoloki wanaunda karibu asilimia 0.9 ya jamii yote ya Ethiopia.Waislamu wa Ethiopia Hali ya Waislamu nchini Ethiopia haikuwa ya kuridhisha katika tawala zilizopita, na kwa hivyo walikuwa wakipewa huduma duni sana za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Pamoja na hayo, lakini kulikuwepo na mabadiliko fulani katika kipindi cha ukaliwaji mabavu wa Ethiopia na askari wa Italia, ambapo Waitaliano walijaribu kuwatumia vibaya Waislamu kwa ajili ya kujidhaminia maslahi yao ya kisiasa. Hata hivyo mabadiliko makubwa yalifanyika katika kipindi cha utawala wa Mengistu Haile Mariam kwa maslahi ya Waislamu. Katika kipindi hicho ambapo kanisa la Orthodox lilikuwa likitawala kila jambo nchini Ethiopia, serikali ya Haile Mariam ilibatilisha haki ya kanisa hilo kuwa mmiliki wa pekee wa ardhi nchini humo.Pia aliongeza siku za mapumziko kwa Waislamu na kutangaza wazi kwamba dini zote zilikuwa sawa mbele ya sheria ya nchi hiyo. Uamuzi huo wa serikali uliwakasirisha baadhi ya viongozi serikalini ambao waliapa kuupinga. Watu wengi wanakiri kwamba kwa kuja madarakani serikali ya PRDEF Waislamu walinufaika na sheria nyingi ambazo walikuwa wamenyimwa katika tawala zilizotangulia.Mojawapo ya haki hizo ni kuruhusiwa kufanya hija. Mabadiliko mengine mazuri yaliyofanywa nchini humo kwa maslahi ya Waislamu ni kuondolewa kwa amri iliyokuwa ikitekelezwa na viongozi wa serikali ya kukaguliwa na kufanyiwa sensa vitabu vya Waislamu na pia kuondolewa kwa marufuku ya kuzuia kuingizwa nchini Ethiopia kitabiu kitakatifu cha Waislamu, yaani Qur'ani Takatifu. Kama ishara ya nia njema kwa Waislamu, Waislamu waliruhusiwa kufanya sherehe zao za kidini na pia kupewa kibali cha kukamilisha maeneo ya ibada na misikiti yao iliyokuwa imepigwa marufuku kujengwa nchini humo katika kipindi cha tawala zilizopita. Hivi sasa mabaraza mawili makuu, la taifa na la Addis Ababa ndiyo yaliyopewa majukumu ya kusimamia na kulinda maslahi ya Waislamu wa Ethiopia. Katika upande wa pili kuna mashirika kadhaa ya Waislamu ambayo yanawahudumia Waislamu na kujaribu kukidhi mahitaji yao kwa njia mbalimbali. Kutokana na maombi ya mara kwa mara ya Waislamu, hivi sasa serikali ya Ethiopia ina mawaziri kadhaa wa Kiislamu ambao baadhi ya wakati hutetea maslahi ya Waislamu.Uhusiano wa kiuchumi wa Ethiopia na Iran Mwanzo wa uhusiano wa kiuchumi na kisiasa wa nchi mbili hizi unaweza kutafutwa katika historia ya kabla ya ...........!