SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 4 Machi 2018

T media news

RC Makonda ahusishwa kufungiwa nyimbo mbili za Diamond

Uongozi wa WCB imezungumzia taarifa za nyimbo mbili za Diamond Platnumz, Waka Waka na Hallelujah kufungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kusema kwamba, wao hawajapewa barua rasmi kuhusu nyimbo hizo kufungiwa.

Hayo yalisemwa na mmoja wa mameneja wa Diamond Platnumz, Sallam SK ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram alieleza kuwa wao hawajapa taarifa rasmi inayoeleza kwanini nyimbo hizo zimefungiwa.

“sioni sababu ya nyimbo ya Hallelujah na Waka kufungiwa kama inavyosemekana maana sisi hatujapata barua ya kuwa nyimbo hizo zimefungiwa na kwa sababu ipi,” aliandika Sallam SK.

Aidha, amesema kuwa wao hawafanyi kazi kwa kukurupuka na kwamba kabla wimbo wowote haujatolewa, basi ni lazima wao na mlezi wa WCB wausikilize kwa makini, na endapo wataridhika nao, basi ndio utatolewa

Ameeleza, kufuatia kuwepo taarifa ya nyimbo hizo kufungiwa, na kama kweli zimefungiwa, basi mlezi wa WCB ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atazungumzia suala hilo zaidi.

“… nyimbo zote za WCB kabla ya kutoka lazima mlezi wetu azipitie, kuna nyimbo nyingi ameshazizuia na zinazotoka basi ameridhia yeye binafsi zitoke. Kama kweli zimefungiwa basi mlezi wetu ataweza kuongea mengi zaidi yangu mimi,” Sallam alihitimisha.

Hivi karibuni TCRA na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) walifungia nyimbo za wasanii nchini huku wengine wakipewa onyo kwa kile walichodai kuwa nyimbo hizo zinakiuka maadili ya kitanzania kutokana na video ama mashairi yake.

Vyombo vya habari vilitakiwa kuachama mara moja kucheza nyimbo hizo.