Mwanzilishi na Mkurugenzi wa mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg jana March 20, 2018 alipokea barua rasmi ya kuitwa kwenye Kamati ya Bunge la Uingereza ili kutoa ushahidi kuhusiana na kampuni yake kuhusishwa na kuweka ushawishi kwenye Uchaguzi wa Urais Marekani, kinyume na sheria.
Sasa leo March 21, 2018 Mwanzilishi Mwenza wa mtandao wa WhatApp Brian Acton amewaambia watumiaji wa Facebook waifute App hiyo na waache kuitumia, jambo ambalo limesababisha hisia tofauti kwa watu mbalimbali.
Acton ametumia mtandao wake wa Twitter kuandika ujumbe unaosema ‘Muda umefika, futeni Facebook’ jambo ambalo baadhi wa watu wamesema ni ‘usaliti wa kibiashara’ kwani Facebook ndiye aliyeinunua WhatsApp na kumtajirisha Acton na Mwanzilishi mwenzie.
Tweet hiyo ya Acton imesababisha kusambaa kwa hashtag ya ‘Futa Facebook’ jambo ambalo linaelezwa kuharibia kampuni hiyo ambayo hadi sasa ina watumiaji zaidi ya milioni 50 duniani kote.
Facebook inatuhumiwa kuruhusu kampuni ya Cambridge Analytica ya nchini Uingereza kutumia taarifa za wanachama wa Facebook Milioni 50 bila ruhusa yao ili kuweka ushawishi katika Uchaguzi Mkuu wa Urais nchini Marekani uliofanyika mwaka 2016 na ili kumpa ushindi Donald Trump.