SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 21 Februari 2018

T media news

Rais Magufuli atoa mil.10/- kwa wananchi Handeni

Rais John Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kuwapatia Sh milioni 10 wananchi wa kijiji cha Kwamkonga wilayani Handeni, mkoani Tanga walizoomba Agosti 3 mwaka jana.

Waliomba fedha hizo kwa ajili ya kuboreshewa huduma za afya katika zahanati ya kijiji hicho iliyokuwa na uhaba wa vifaa tiba.

Rais Magufuli alipita katika kijiji hicho kilichopo pembezoni mwa barabara ya Chalinze-Segera na kuzungumza na wananchi hao wakati akielekea mjini Tanga kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Chongoleani mkoani Tanga hadi Hoima nchini Uganda.

Wananchi hao walimweleza Rais matatizo mbalimbali inayoikabli zahanati yao hasa suala la maabara ambayo walikuwa wakikosa huduma hizo hadi wazifuate katika kituo cha afya Mkata au kwenda katika hospitali ya wilaya Handeni.

Akikabidhi kwa niaba ya Rais, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema Rais alipopewa malalamiko na wananchi kuhusu kuboreshwa zahanati hiyo, ameleta kiasi cha milioni 10 ambacho kimetumika kununua vifaa mbalimbali vinavyopaswa kuwekwa kwenye maabara.

Shigela alisema Rais anajali wananchi wake waliomchagua ndiyo maana ameweza kuleta fedha hizo ili wapatae huduma karibu na vijiji vyao kwa lengo la kupunguza safari za kwenda umbali mrefu kufuata huduma za maabara.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Handeni, Dk Credianus Mgimba alisema walipopokea fedha hizo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga, waliziweka katika akiba ya zahanati ya kijiji hicho ambapo walifanya manunuzi ya vifaa hivyo.

Akitoa shukrani Mkuu wa wilaya hiyo, Godwin Gondwe alimshukuru Rais kwa kutekeleza ahadi hiyo ambayo itawawezesha wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani kupata huduma bora za afya hasa za maabara na kupunguza msongamano katika vituo vya afya na hospitali ya wilaya.