VIONGOZI mbalimbali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanatarajia kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Katibu wa Chama hicho kata ya Hananasifu, Daniel John.
Daniel alikutwa amefariki dunia kwenye ufukwe wa Coco, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam huku mwili wake ukiwa na majeraha na inadaiwa alitekwa na watu wasiojulikana akitokea katika shughuli za kampeni za uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni.
Taarifa kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, jana ilieleza kuwa mwili wa marehemu John unatarajiwa kuzikwa kesho mkoani Iringa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwili utapelekwa Kanisa Katoliki Hananasifu kwa ajili ya misa ya kumuombea marehemu itakayoanza saa 5.00 asubuhi.
“Viongozi wa chama, wakiwemo wakuu na waandamizi, wanatarajiwa kuongoza shughuli ya utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Katibu wa Chama Kata ya Hananasifu, Jimbo la Kinondoni, Kamanda Daniely John, itakaofanyika kesho (leo), jijini Dar es Salaam,” alisema Makene.
Alisema baada ya ibada, waombolezaji watatoa heshima za mwisho na baadaye mwili kusafirishwa kwenda mkoani Iringa ambako atazikwa katika kijiji cha Chikelewatu wilayani Mafinga.
Aidha, Chadema imetoa wito kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kutoa heshima zao.
Juzi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliweleza waandishi wa habari kuwa uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa kada huyo wa Chadema unaendelea vizuri, na kwamba hadi sasa Jeshi la Polisi limeshamkamata shahidi mmoja ambaye anatoa ushirikiano mzuri.
Masauni alisema pindi uchunguzi utakapokamilika, taarifa itatolewa kwa wananchi ili wafahamu ukweli wa tukio hilo ambalo limeleta sintofahamu kwa jamii.