SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 28 Februari 2018

T media news

Aliyemuhukumu Sugu Achukua Likizo

Hakimu Michael Mteite aliyemhukumu kifungo cha miezi mitano jela mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ameanza likizo jana.

Mteite, ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, alitoa hukumu hiyo juzi kwa Sugu pamoja na katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga baada ya kuwatia hatiani kwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Sugu na Masonga walitoa kauli hiyo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Hakimu huyo alipopigiwa simu jana na mwandishi wa Mwananchi aliyetaka kujua kuhusu uwepo wake likizo, kabla hata ya kuelezwa hilo alimtaka kuwasiliana na Msajili wa Mahakama.

Hata alipotumiwa ujumbe wa maneno (sms) kujulishwa kwamba msajili alishalizungumzia hilo na kilichohitajika ni kauli yake, hakujibu.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, naibu msajili mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, George Herbert alisema Hakimu Mteite amechukua likizo kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa utumishi kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma pindi muda wao unapokuwa umefika.

“Ni likizo yake ya mwaka… na amechukua likizo kama mtumishi mwingine ambaye anaweza kuchukua likizo muda wake unapokuwa umefika. Kimsingi ni kwamba amechukua likizo ya muda wa wiki tatu kuanzia leo (jana) na ni likizo huwa anachukua kila mwaka muda unapokuwa umefika.

“Hivyo suala la kusema kwamba eti amechukua likizo kwa sababu ya hukumu aliyoitoa jana (juzi) haina msingi wowote, bali ni haki yake kuchukua likizo hiyo. Inapofika Februari kila mwaka huchukua likizo yake na huwa inategemea majukumu anayokuwa amepangiwa kuyafanya,” alisema naibu msajili.

Taarifa ya kusudio la rufaa

Akizungumzia taarifa ya kusudio la mawakili wa Sugu na Masonga kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo na kuomba dhamana kwa wateja wao, Naibu Msajili Mfawidhi, Herbert alisema baada ya hukumu kutolewa juzi, mawakili hao walianza mchakato wa kukata rufaa na siku hiyohiyo walipatiwa nakala ya hukumu.

Alisema kilichokuwa kikisubiriwa hadi jana ni nakala za mwenendo wa kesi ili kukamilisha utaratibu wa kukata rufaa.

Herbert alisema kukata rufaa ni haki ya mlalamikaji anapoona hajaridhishwa na hukumu.

Alisema, “Kinachofanyika ni kuhakikisha wanapatiwa mwenendo wa shauri na hilo lipo hatua za mwisho kukamilika kwa sababu wameshapata nakala ya uamuzi ulitolewa jana ileile,” alisema.

Mke wa Sugu, Masonga walonga

Happy Msonga ambaye ni mke wa Sugu na Grace Mallya wa Masonga wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema wanajua fika hukumu ilitolewa kwa mrengo wa kisiasa, hivyo hawakubaliani na adhabu waliyopewa waume wao.

Grace alisema, “Ukiachilia mbali ndani ya familia tu, lakini wale watu wa nje wanavyo ‘comment’ unaona kabisa hakuna haki iliyotendeka.”

Alisema anazidi kumuombea mume wake aendelee kuwa na nguvu na imara zaidi katika kipindi chote anachopitia kwa kuwa ana imani hayo ni mapito na yatakuwa na mwisho ambao huwa ni ukombozi katika harakati za kisiasa.

Happy alisema walitarajia kilichotokea kwa kuwa walishaona dalili mwanzoni baada ya hakimu kukataa kujitoa wakati washtakiwa walishamkataa.

Alisema wana imani na mawakili, Peter Kibatala na Faraji Mangula kwamba watafanikiwa kukata rufaa kwa ajili ya uamuzi mwingine. Alisema kwa sasa wanawaombea kwa Mungu, Sugu na Masonga waendelee kuwa na afya njema.

Wakati Sugu akitumikia adhabu ya kifungo, mama yake mzazi Desderia Mbilinyi imeelezwa na familia kuwa ni mgonjwa.

Wasemavyo wapigakura Mbeya

Akizungumzia hukumu iliyotolewa kwa Sugu na Masonga mkazi wa Uyole, Bahati Longopa alisema Mahakama imetenda haki kulingana na vifungu vya sheria. Hata hivyo, alisema ni vyema ingetoa hukumu ya kifungo cha nje ili mbunge huyo aweze kuwatumikia wananchi katika shughuli za maendeleo.

Mkazi wa Sabasaba, John Mbika alisema ni mapema kuzungumzia hilo hivyo ni vyema Mahakama ikaachiwa iendelee na kazi.

Mkazi wa Nonde, Rehema Mwanjonde alisema Mahakama imetenda haki kwa mujibu wa sheria lakini akaitaka Chadema ikate rufaa ili Sugu aweze kuwatumikia wananchi na kusimamia shughuli za maendeleo.

Hoja sita za Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akizungumzia hukumu hiyo katika waraka alioutoa juzi aliibua hoja sita.

Lissu anayeendelea na matibabu nchini Ubelgiji katika hoja ya kwanza alisema hukumu hiyo si mwisho wa mjadala mahakamani na kwamba bado kuna fursa na haki ya rufaa Mahakama Kuu na ikibidi Mahakama ya Rufaa.

Pili, alisema hukumu hiyo haina maana Sugu atakaa gerezani muda wote, kwamba kuna haki ya dhamana (pending appeal) na kubainisha kuwa hivyo ndivyo walivyofanya kwa viongozi na wanachama wengi wa Chadema.

Katika hoja ya tatu, Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema alisema hukumu ya Sugu haina athari yoyote kwa mbunge huyo kuhusu kugombea tena au kupoteza ubunge wake kwa sababu Katiba inaweka masharti ya kifungo cha miezi sita au zaidi na kwa makosa ya utovu wa uaminifu.

“Uchochezi au kutoa lugha ya matusi sio makosa ya utovu wa uaminifu,” alisema.

“Nne, pamoja na kwamba sijaona nakala ya hukumu, adhabu ya kifungo bila faini kwa kosa la kwanza ni kinyume na ‘sentencing principles’. Hii ni mojawapo ya hoja zetu zilizoshinda katika kesi ya Peter Lijualikali (mbunge wa Kilombero) Mahakama Kuu mwaka jana,” alisema.

Tano, Lissu alisema hata kama Sugu atakaa gerezani muda wote huo (wa miezi mitano), hukumu za kesi za kisiasa kama hiyo hazijawahi kuwapunguzia heshima wapigania haki popote duniani.

Jambo la sita alisema, “Naunga mkono pendekezo la Zitto (Kabwe-mbunge wa Kigoma Mjini) kwamba wabunge wetu wote warekodi maneno aliyofungiwa nayo Sugu na kuyaweka mitandaoni ili watukamate na sisi pia, mpaka wakimbie wenyewe au watukamate na kutufunga wote.”