SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 20 Novemba 2017

T media news

Alichokisema Nyalandu baada ya kujiunga rasmi na CHADEMA

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), LAzaro Nyalandu, jana amaejiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na MAendeleo (CHADEMA) ambapo alikabidhiwa kadi ya chama hicho na mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Nyalandu ambaye alijivua uanachama wa CCM na kujiunga na CHADEMA alieleza luwa amejiunga na chama hicho ili kupigania haki pamoja na kuhamasisha mjadala wa mabadiliko ya katiba.

“Nitaungana na wanaharakati wote tufanye rejea ya rasimu ya mabadiliko ya katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Mabadiliko ya kisiasa ni lazima nchini Tanzania na wakati ni huu,” alisema Nyalandu.

Nyalandu aliongeza kuwa atakuwa mwaminifu katika kuitumikia nchi ya Tanznaia na kuwataka wananchi wote kuungana kwa pamoja ili kuipigania haki.

“Daima nitakuwa mwaminifu kwa nchi yangu ya Tanzania na kwamba naungana na Upinzani kwa kuwa nina nia thabiti ya kupigania haki. Na kwa kuwa sote tunajua imeandikwa tangu zamani kwamba haki huinua taifa na kwa kuwa tukiungana kama taifa tunaweza kufanya mambo ambayo hayawezi kufanywa na mtu mmoja mmoja,” alisema.

Lazaro Nyalandu ambaye alikuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alijivua nafasi hiyo pamoja na nafazi nyingine zote alizokuwa anazishikilia katika chama hicho pamoja na kujivua uanachama kutokana na sababu alizozitaja kuwa ni hali mbaya ya kisiasa, ukiukwaji haki za binadamu, dhuluma, kuingiliana mihimili ya dola pamoja na CCM kupoteza mwelekeo.