Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amemjibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe. Jaji Francis S.K.Mutungi kuhusu sakata la kufukuzwa uanachama wanachama saba wa CUF na kuhusu kutomtambua yeye kama Katibu wa CUF.
Maalim Seif amedai kuwa wao kama CUF hawakubaliani na maamuzi ya Jaji Mutungi kumtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF kwa kuwa wao tayari walishamfukuza uanachama hivyo si mwanachama wa CUF na wala hana sifa ya kuwa kiongozi katika chama hicho.
"Mheshimiwa Msajili unafahamu fika kuwa Profesa Ibrahim H. Lipumba mwenyewe aliamua kujiuzuilu uenyekiti wa taifa wa Chama cha CUF. Pamoja na kuniandikia mimi nikiwa Katibu Mkuu na pia Katibu wa Mamlaka iliyomchagua (Mkutano Mkuu wa Taifa) kunijulisha kuwa amejiuzulu, pia alikwenda kwenye mkutano na waandishi wa habari akatangaza hadharani kuwa amejiuzulu
"Hatimaye Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF ukaitishwa na Katibu Mkuu akatoa taarifa ya kupokea barua ya kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba nafasi yake ya Uenyekiti wa Taifa wa Chama. Nikaisoma barua yake mbele ya Mkutano Mkuu wa Taifa, na baada ya mjadala wa kina maamuzi yakachukuliwa kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) kwa kupiga kura. Wajumbe 437 wakakubali kujizulu kwa Profesa Lipumba dhidi ya Wajumbe 14 waliokataa. Hivyo Profesa Ibrahim H. Lipumba kuanzia siku aliyojiuzulu si Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Profesa Lipumba hana mamlaka ya kukiongoza Chama chetu" alisisitiza
Aidha Maalim Seif anasema kutokana na maamuzi hayo ya CUF baadaye Profesa Lipumba alikuwa akilalamika kwa Msajili wa Vyama Vya Siasa kufuatia maamuzi hayo na baadaye Msajili alitoa msimamo wake kuwa anamtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ingawa Katibu Mkuu wa CUF anasema msajili hana uwezo huo wa kumrudisha Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF
"Najua kuwa alikulalamikia, ukaniletea barua zake za malalamiko na ukataka maoni ya Chama. Nikakujibu kwa maandishi. Kwenda na kurudi ukatoa kile ulichokiita Msimamo wa Msajili juu ya kadhia iliyokikumba Chama! Huo ni Msimamo sio hukumu. Maana kama ni hukumu ningetarajia katika huo ulioita msimamo ungeeleza kuwa kwa uwezo uliopewa na kifungu Na. kadhaa cha Sheria ya Vyama vya Siasa Na.5 ya 1992, au kwa mujibu wa uwezo uliopewa na Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) katika kifungu Na. kadhaa umeamua kumrudisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Lakini hukuweza kuonyesha uwezo wako wa kisheria au kikatiba kumrudisha Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa CUF kwa sababu huna uwezo huo kwa mujibu wa sheria za nchi wala kwa mujibu wa Katiba ya CUF" alisema Maalim Seif
Katibu Mkuu wa CUF amesema wao wanazidi kumshangaa msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Mutungi kuendelea kushirikiana na Profesa Lipumba hata katika mambo ambayo yanatia aibu kama kutaka kutoa ruzuku za chama na kumpa Lipumba na genge lake.
"Tunaloshuhudia ni kila kukicha unaendelea kumuunga mkono Profesa Lipumba hata katika mambo ya aibu ya kula njama na Profesa Lipumba kumuwezesha atoe ruzuku ya CUF kinyume na matakwa na taratibu zilizowekwa katika Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014). Narudia kusema kuwa Prof. Lipumba si Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Lakini kutokana na vitendo vyake vya kukosa nidhamu katika kusababisha vurugu katika kikao cha dharura cha Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama chetu, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kwa uwezo lillonao kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya CUF, lilimfukuza Profesa Ibrahim Lipumba uanachama wa CUF. Taarifa hiyo pia nilikuletea, lakini umeamua kuitia kapuni ili kutimiza matakwa yako binafsi. Ikiwa Profesa Ibrahim H. Lipumba sio mwanachama wa CUF, hawezi kabisa kuwa kiongozi wa Chama, hasa nafasi ya juu kabisa katika Chama. Kinachotokea kikiongozwa nawe na Ofisi yako ni ubabe, kutojali sheria za nchi wala Katiba ya Chama chetu ilimradi mufikie lengo lenu" alisema Maalim
Mbali na hilo Maalim Seif aliweka msimamo wake kuwa Chama Cha Wananchi CUF hakiendeshwi na hisia za mtu wala hakiwezi kupangiwa kiongozi na kudai ni CUF ni taasisi inayoongozwa na sheria za nchi na Katiba na si vinginevyo.
"Mheshimiwa Msajili napenda utambue kuwa CUF ni taasisi, tena Taasisi makini. Kinaendeshwa na kuongozwa kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya Chama hicho pamoja na Kanuni ambazo hutungwa na mamlaka husika kila inapohitajika. Sisi viongozi wa CUF tunajitahidi kuongozwa na sheria za nchi, Katiba ya Chama na Kanuni zake katika kukiendesha chama. Hatuongozwi na matakwa ya mtu yeyote, hata kama mtu huyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa. Ninavyofahamu Msajili hana mamlaka ya kupandikiza watu anaowataka kuwa viongozi wa chama chetu. Msajili hana uwezo wa kuingilia maamuzi halali ya vikao halali vya Chama chetu. Viongozi huchaguliwa /kuteuliwa na wanachama wenyewe/viongozi halali wa chama"alisisitiza Maalim Seif