SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 24 Desemba 2016

T media news

SAMIA AWATAKA WAZAZI WALEZI ZNZ KUACHA TABIA YA KUWAOZA WASICHANA KATIKA UMRI MDOGO..!!!

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi wa visiwani Zanzibar, kuacha tabia ya kuwaoza wasichana wakiwa na umri mdogo, bali wawasomeshe kwa ajili ya manufaa yao ya jamii kwa ujumla.

Samia alisema hayo kwa nyakati tofauti, wakati akizindua madarasa ya kisasa iliyojengwa kwenye eneo la Kilimani na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa msikiti mkubwa kuliko yote nchini Tanzania unaojengwa katika eneo la Ijitimai Kidoti mkoani Kaskazini Unguja.

Ujenzi huo unafanywa kwa michango ya wananchi. Alisema hayo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya Kikazi Unguja.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Zanzibar, ilieleza kuwa makamu huyo wa Rais yupo katika ziara visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Samia alisema kama wazazi na walezi watasomesha watoto wa kike, elimu watakayopata itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana hao, kufanya maamuzi sahihi na yenye tija katika jamii.

Alisisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa mtoto wa kike, hivyo ni muhimu kwa jamii ya Zanzibar ihakikishe watoto wa kike wote wanapata elimu, kwani watakuwa na uwezo wa kuchagua na kuandaa mustakbali wa maisha yao ya baadaye, ikilinganishwa na hali ilivyo sasa kwenye baadhi ya maeneo

Kuhusu elimu ya dini, aliwahimiza wazazi na walezi, kuwalea watoto katika maadili mema kwa kuzingatia maandiko matakatifu ya Mtume Mohammad (S.A.W).