Watu wawili wamefariki dunia na wengine zaidi ya 26 wamejeruhiwa na kulazwa katika hosipitali ya mkoa wa Singida baada ya basi la kampuni ya National Express lililokuwa likitokea Iramba kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika wilaya ya Mkalama.
Mganga mkuu wa hosipitali hiyo daktari John Mwombeki amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na amesema amepokea majeruhi 26 na maiti 2 moja ni ya dereva wa basi hilo bwana Athuman Said na nyingine ni ya mama aliyetambulika kwa jina la Janeth ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Maluga wilayani Iramba.
Kamanda polisi mkoani Singida kamishna msaidizi wa polisi ACP Debora Daudi Magiligimba amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva na kutokufuata sheria za barabarani na kusisitiza madereva kuwa makini ili kuepukana na ajali za kizembe kama hizi.