Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kote nchini ili kuwajengea wananchi uelewa sahihi juu majukumu ya Tume na chaguzi zinazofanyika nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Jaji Lubuva amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kutimiza Haki yao ya Kikatiba ya kupiga Kura kuwachagua viongozi wananowapenda kwa sababu ya kukosa uelewa juu ya Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia Uchaguzi .
Amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inaipa NEC jukumu la kusimamia na kuendesha Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara na kubainisha kuwa ili jukumu hilo lifanywe kwa ufanisi wananchi waliotimiza vigezo vya kupiga kura na wale wanaotarajia kupiga kura miaka ijayo lazima wapatiwe elimu sahihi ya Mpiga Kura.
Amefafanua kuwa baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015, NEC ilianza kutekeleza programu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya Mpiga Kura kuwafikia wananchi moja kwa moja kupitia mikutano mikubwa inayohusisha viongozi mbalimbali, maonesho ya Sabasaba na Nane Nane , kutoa elimu ya Mpiga kura kwenye vyombo mbalimbali vya habari pamoja na kuzitembelea baadhi ya shule za Sekondari za mkoa wa Singida na Mara.
” Moja ya shughuli za Tume ni kuendesha na kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara, ili shughuli hii tuifanye vizuri ni muhimu sana tuwapatie wananchi elimu sahihi juu ya upigaji wa kura, tutafanya jambo hili tukishirikiana na wadau na Asasi nyingine ambazo tutazipa kibali cha kutoa elimu hii”Amesisitiza Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva amebainisha kwamba utoaji wa elimu hiyo utaongeza idadi ya wapiga kura kwenye chaguzi zijazo akitoa mfano wa idadi pungufu ya wapiga waliojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na ule uliofanyika Oktoba 25 , 2015 ambapo baadhi ya wananchi walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la Wapiga Kura na kupewa vitambulisho hawakujitokeza kupiga kura.
” Tunalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia umuhimu wa wananchi kushiriki Kupiga Kura, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijitokeza ili wapate vitambulisho jambo ambalo sio sahihi, mfano mwaka 2010 wananchi milioni 15 walijiandikisha kupiga kura lakini waliojitokeza kupiga kura ni milioni 8.626 hii ni idadi ya chini, pia mwaka 2015 wananchi waliojiandikisha walikuwa milioni 23,161,440 lakini waliojitokeza Kupiga Kura ni watu milioni 15,589,639 hapa kuna ongezeko, tunaamini tukiwapatia elimu wengi zaidi watajitokeza kuwachagua viongozi wanaowapenda ” Amesitiza Jaji Lubuva.
Amesema katika kuendelea kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi wengi zaidi NEC itashiriki Kongamano na maonesho ya Wiki ya Vijana yatakayoambatana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2016 Oktoba 7 hadi 14, 2016 mkoani Simiyu ambapo pamoja na Mambo mengine watendaji na Maafisa wa Tume watatoa elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi na kutembelea shule za Sekondari za mkoa huo.
Aidha, ili kuboresha chaguzi zijazo ametoa wito kwa wananchi waendelee kushirikiana na Tume kwa kujitokeza kwa wingi kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa hoja mbalimbali katika maeneo ambayo watendaji wa NEC watafika kutoa elimu ya Mpiga Kura.
Na Aron Msigwa – NEC