KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Sirro amesema jeshi hilo limemkamata mtuhumiwa ‘Scopion’ aliyehusika katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha eneo la Buguruni jijini humo.
Sirro alitoa kauli hiyo jana Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kujadili usalama katika eneo hilo ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Alisema mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina maarufu kama Scopion alikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa za matukio ambayo ameyafanya ikiwemo la kumchoma kisu, kumtoa macho na kumsababishia upofu, Said Ally.
"Nimesikia wananchi wanalalamika hapa kuwa tumeshindwa kumkamata Scopion, ni nani kwa Jeshi la Polisi asikamatwe, tayari tumemkamata na sheria itachukua mkondo wake, hakuna mtu anayeweza kushindana na jeshi," alisema.
Aidha Sirro alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo na kuhojiwa aliutaja mtandao wake wote na tayari wameukamata, hivyo amewataka wakazi wa eneo hilo kutokuwa na hofu kwani mtuhumiwa huyo hayupo tena katika eneo hilo.
"Najua suala hili bado lipo mahakamani hatuwezi kulizungumzia sana, bahati nzuri alipokamatwa alieleza aliyoeleza na tukafanikiwa kuukamata mtandao wote, hivyo hakuna haja ya kuwa na uwoga eneo hili lipo salama," alisema.
Kabla ya kauli hiyo ya Sirro, wananchi wamelalamikia askari wa eneo hilo ambao walishindwa kuchukua hatua kwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifahamika muda mrefu. Sadiki Mgaya ambaye alishuhudia tukio la kuchomwa kisu na kutolewa macho kwa Said Ally, alisema mtuhumiwa huyo alisema kuwa amekuja kwa ajili ya kulipa kisasi kwa wakabaji baada ya yeye kukabwa.
Alisema baada ya kufanya tukio hilo, askari walifika katika eneo hilo na mtuhumiwa huyo akiwa hapo na wananchi waliwaonesha askari lakini hawakuchukua hatua zozote badala yake waliwataka wananchi wamkamate.
Aidha wananchi hao pia wamemlalamikia Mkuu wa Kituo cha Polisi Mnyamani na kudai kuwa amekuwa akipelekewa taarifa za uhalifu ikiwemo za vibaka lakini mtu anapokamatwa akifika kituoni hapo anatoa rushwa na kuruhusiwa kuondoka.
Lakini akiondoka askari wengine wanatumwa tena kumkamata. Kauli hizo za wananchi zikamfanya Sirro kutoa kauli ambapo alisema askari na maofisa wote ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na kufukuzwa kazi.
"Najua wapo askari na maofisa wa ovyo ambao hawajui kutimiza wajibu wao, lakini nikuahidi Mkuu wa Mkoa tutawachukulia hatua, nimesikia hapa wananchi wanalalamika askari wanachukua rushwa, tutachunguza tukijiridhisha basi ni lazima tuchukue hatua," aliongeza.
Aidha Sirro alisema watafanya doria kubwa katika eneo hilo ili kuwakamata wote wanaohusika na matukio ya kihalifu kwani wamebaini katika eneo hilo bado kuna uporaji mdogo mdogo.
"Tutarudi hapa tunaomba ushirikiano wenu bila ninyi kutuambia hatuwezi kujua, nawaomba wazazi muwakanye watoto wenu ambao wanahusika na matukio hayo kwani tutakapoanza msako huo wasije wakalalamika, uhalifu haulipi na mwisho wa siku utamkosa mtoto wako," alisisitiza.
Kwa upande wake Makonda aliwataka wananchi hao kujitolea kufanya ulinzi shirikishi na kuwataka wananchi kuchangia ulinzi huo ili vijana hao wahusike kufanya ulinzi na kulifanya eneo hilo libaki na amani.
"Tuna wajibu wa kufanya ulinzi shirikishi wananchi mtoe michango, hapa Sirro amesema mapungufu yaliyopo kwenye vituo yanafanyiwa kazi, niwaase tu mjiepushe na matukio ya kuhalifu kwani wale watakaokamatwa sheria itachukua mkondo wake," alisema Makonda.