Kiungo wa Roma, Radja Nainggolan amewalalamikia mashabiki wa klabu yake kwamba hawawashangilii ipasavyo mpaka pale Francesco Totti anapoingia uwanjani.
Kocha wa Roma, Luciano Spalletti alisema baada ya ushindi wa 3-2 Jumapili dhidi ya Sampdoria – ikiwa ni mechi ambayo Totti alitokea benchi na kufunga goli la ushindi dakika ya mwisho – kwamba klabu inahitaji kiongozi mwingine pamoja na nahodha.
Nainggolan anaamini anaweza kuwa kiongozi mpya, japo bado anaona mashabiki wa Roma inabidi watimize majukumu yao kwa kuishangilia kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
“Najiona kama kiongozi wa hii timu”, alinukuliwa na Gazzetta dello Sport. “Ninakubali kwamba katika kipindi cha pili (dhidi ya Sampdoria) timu ilikuwa tofauti: pale Totti alipoingia, kulikuwa na shauku ya tofauti kabisa kwa mashabiki.
“Ninashangaa kwa nini katika kpindi cha kwanza, wakati tulipokuwa nyuma kwa goli 2-1, kitu kilichosikika ni filimbi na kuzomewa. Ni ngumu kucheza kwa utulivu na kujiamini katika hali kama hiyo – Totti alipoingia tulihisi kupata nguvu sana.”
Wakati huohuo, kiungo wa zamani wa Roma, Olivier Dacourt amesema kuwa siri ya mafanikio ya Totti ni uwezo wa kuona mambo kabla ya wengine.
