Waziri wa elimu nchini Sweden amejiuzulu wadhifa wake baada ya kupatikana akiendesha gari akiwa mlevi.
Bi Aida Hadzialic, ambaye amekuwa waziri wa elimu ya sekondari na elimu ya watu wazima, amejiuzulu baada ya kukamatwa na polisi Malmo.
Kwenye taarifa iliyoonyesha hisia nyingi, Bi Hadzialic , ambaye ndiye mtu mchanga zaidi kuwahi kuteuliwa waziri nchini humo, amesema sharti awajibike kwa alichosema ni kosa kubwa zaidi alilowahi kulifanya maishani mwake.
Alipimwa na kugunduliwa kwamba alikuwa tu amepitisha kidogo kipimo kinachoruhusiwa cha unywaji pombe.
Sweden huwa na sheria kali sana za kuzuia uendeshaji gari mtu akiwa amelewa.
Bi Hadzialic, aliyehamia Sweden kama mkimbizi Mwislamu kutoka Bosnia Herzegovina akiwa mdogo, amesema alikuwa amekunywa gilasi mbili pekee za mvinyo.