SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 29 Julai 2016

T media news

Taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu kuvamiwa kwa shirika lililokuwa likigawa vilainishi Shinyanga

Wizara imepokea taarifa kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Shinyanga imevamia ofisi za shirika la Jhpiego mkoani humo na kukamata baadhi ya watumishi wake kwa madai ya shirika hilo kugawa mafuta maalumu yanayodhaniwa kutumiwa kuhamasisha ngono za jinsia moja. Baada ya taarifa hiyo wizara inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:

Si kweli kwamba shirika la Jhpiego limekuwa likihamasisha ngono baina ya wapenzi wa jinsia moja. Shirika hilo kupitia mradi wa “Sauti” linasaidia serikali katika jitihada za kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa makundi yaliyopo kwenye hatari kubwa ya maambukizi. 

Moja ya makundi yanayolengwa ni wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao. Shirika limekua likitoa elimu ya mabadiliko ya tabia kwa wanaume hao huku likiwapatia mafuta hayo kama sehemu ya kuwasaidia kupunguza hatari ya maambukizi.

Mafuta hayo yaliingizwa nchini kwa kufuata taratibu za kisheria kwa ufadhili wa Mfuko Maalumu wa Rais wa Marekani wa kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI (PEPFAR).

Ndugu wanahabari, kama mtakumbuka hivi karibuni Wizara kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ilisitisha ugawaji wa mafuta hayo maalumu (vilainishi) miongoni mwa makundi hayo maalumu.

Kufuatia agizo hilo, Wizara iliagiza Shirika hilo kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi za PEPFAR zilizopo Ubalozi wa Marekani ili yapelekwe katika nchi nyingine zinazofadhiliwa na PEPFAR ambazo matumizi ya mafuta hayo hayajazuiwa.

Ndugu wanahabari, Shirika hilo lilitekeleza agizo la wizara la kukusanya mafuta hayo na kuyaweka katika ofisi zao za kanda, tayari kuyasafirisha kuja jijini Dar es Salaam, ambapo umeandaliwa utaratibu maalumu wa kuyapeleka katika nchi nyingine bila kuyaharibu.

Mnamo tarehe 27 mwezi July, mwaka 2016 Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga ilivamia Ofisi za Shirika hilo na kuchukua mafuta hayo bila kuelewa utaratibu uliotolewa na Wizara wa kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi za PEPFAR.

Zoezi hilo la kamati ya Ulinzi na Usalama halikushirikisha wizara ya Afya wala wadau wa sekta ya Afya wilayani humo, ambao wanaelewa vizuri utaratibu uliowekwa na wizara kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha mahali husika bila kuyaharibu.

Ndugu wanahabari, tayari Wizara imeshamuandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kutaka mafuta hayo yaliyochukuliwa kurudishwa katika ofisi za mradi wa Sauti zilizopo mtaa wa Mwasele, kata ya Kambarage mkoani Shinyanga ili zoezi la kuyakusanya na kuyarudisha Dar es Salaam liweze kuendelea.

Mwisho, Wizara inapenda kuwajulisha kuwa shirika la Jhpiego ni miongoni mwa wadau wakuu wa Serikali ambao wamekuwa wakisaidia huduma mbalimbali za Afya nchini ikiwemo kusaidia ujenzi wa vituo vya afya, kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kuboresha Afya ya mama na mtoto na Uzazi wa Mpango kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Hivyo serikali imeridhia shirika hilo kuendelea kutoa huduma mbalimbali za afya bila kutumia mafuta hayo.

Imetolewa na:

Michael O. John

Kaimu Katibu Mkuu,

Wiza ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.