Mtunzi: Enea Faidy
.....EDDY aliumia sana kwa taarifa zile za kifo cha mama yake. Hakutaka kuamini kama kweli mama yake hatakuwa pamoja nao tena. Machozi yalimbubujika kwa kasi huku akimwita mama take kana kwamba alikuwa karibu yake.
Mr.Alloyce alishindwa kuvumilia, alijikuta akiungana na mwanaye kulia. Walilia sana mpaka machozi yaliwakauka, Mr Alloyce alichukua leso yake na kujifuta machozi yake kisha akachukua simu ili awajulishe ndugu na marafiki kuhusu kifo cha mkewe.
Moyo wake ulisita sita sana kwani aliwaza ni jinsi gani ndugu wangeupokea msiba ule wa ghafla bila hata maiti.
"Eddy watanielewaje shemeji zangu? Umesababisha yote haya mwanangu, lakini siwezi kukulaumu!" Alisema Mr Alloyce huku machozi yakimlengalenga.
"Nisamehe dady kwa kuwa chanzo cha matatizo yote!" Alisema Eddy na kuendelea kulia.
Lakini hawakuwa na jinsi ya kufanya kwani tayari maji yalikwisha mwagika na ilikuwa vigumu sana kuzoleka. Ilibidi wakubaliane na kilichotokea ingawa kishingo upande sana.
Mr Alloyce alitafuta namba kwenye simu yake, MTU wa kwanza kumpata alikuwa shemeji yake aishiye jijini Dar ( Dada wa mama Eddy). Simu iliita kisha ikapokelewa, kwa kitete na woga Mr Alloyce akaanzisha mazungumzo.
"Halloo Shem"
"Niambie Shem wake mie.. Kwema huko?" Alisema shemeji yake Alloyce kwa uchangamfu sana kama ilivyokuwa kawaida yake. Hakuijua msiba mzito uliokuwa moyoni mwa Mr.Alloyce.
"Huku sio kwema Shem..!" Aliens Mr Alloyce.
"Sio kwema kuna nini?" Alishtuka.
"Sio kwema naomba kesho mfike nyumbani kwangu tafadhali.."
"Kuna nini shemeji? Naomba niambie tu.. Nini kimetokea?"
"Utajua kila kitu kesho..!"
"Hapana..niambie Leo.. Au MPE mama Eddy simu niongee nae..!" Maneno hayo yalimkata maini Baba Eddy hakuelewa ajibu nini akabaki kimya kwa sekunde chache akitafakari cha kujibu lakini ghafla akasikia sauti Kali ya Eddy ikimwita."Daaaaaaaaady!"
Mr Alloyce alishtuka sana kwani Eddy alikuwa ametoka sebuleni pale dakika chache zilizopita wakati yeye akiongea na simu. Hofu ikamkamata ghafla na kumfanya Mr Alloyce atupe simu sofani na kuelekea sauti ya Eddy inakotokea. Eddy aliita tena "Daaaaaaaady!" Mara hii sauti ile iliambatana na mwangwi mkali uliozidi kumtisha Mr Alloyce.
Alitoka sebuleni na kwenda koridoni lakini hakumuona Eddy. Akasikia sauti ikitokea chooni, alikimbia haraka na kwenda chooni lakini hakumuona, ghafla sauti ya Eddy ikasikika tena ikitokea chumbani kwa Eddy ilibidi amfuate haraka lakini cha kusikitisha Mr Alloyce hakumkuta Eddy ila alikuta damu nyingi zikiwa sakafuni. Alishtuka sana.